Habari Mseto

Ramadhani: Wachuuzi wa vyakula wakwepa hasara mbunge wa zamani akivinunua

March 18th, 2024 2 min read

NA CHARLES ONGADI 

KUFUATIA hali ngumu ya maisha wafanyabiashara wa mapato ya chini na ya kadri hususan mashinani wamekuwa wakipitia nyakati ngumu, hasa kipindi hiki uchumi unazidi kuwa ghali.

Ni jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limeathiri biashara zao, idadi ya wateja ikipungua.

Aghalabu, wafanyibiashara hao hasa wa bidhaa za kula hukadiria hasara wanapokosa wanunuzi a kupelekea biashara zao kuyumba.

Nyakati zingine, wanaishia kutupa bidhaa zao zinapoharibika kwa sababu ya kukosa miundomsingi faafu kakam vile friji.

Hata hivyo, akina mama wanaouza vyakula mtaani Mjambere Barani katika eneoubunge la Kisauni Kaunti ya Mombasa, waliangukia bahati ya mtende mnamo Jumapili, Machi 17, 2024.

Katika tukio lisilo la kawaida, wafanyabiashara hao wanaouza vyakula kandokando mwa barabara kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani waliweza kufunga biashara zao mapema baada ya vyakula vyao kununuliwa vyote.

Aliyekuwa Mbunge wa eneo la Kisauni Ali Menza Mbogo aliwashangaza, japo kwa tabasamu, aliponunua vyakula vyao ili kusambazia waumini wa dini ya Kiislamu wanaoendelea na mfungo wa Ramadhani.

Waumini wa dini ya Kiislamu eneo la Mjambere Bomani walinufaika kwa vyakula hivyo walivyotumia kufungua kula wakati wa jioni.

Ofa hiyo ya chakula ilikuwa ni afueni kwao hasa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayozidi kung’ata nchini.

Wengi wakiwa wachuuzi wa mahamri, kaimati, mbaazi, mihogo, samaki wa kupakwa na aina tofauti ya mapochopocho, walimshukuru Bw Mbogo kwa hatua aliyochukua inayoashiria upendo alio nao kwa wananchi hasa wakati huu mgumu wa kiuchumi.

Baadaye mbunge huyo wa zamani alijumuika na wazee kwa vijana wa mtaa huo kula chakula cha jioni.

“Tumetembea mitaani tukinunua vyakula kutoka kwa akina mama hawa wafanyibiashara kwa minajili ya ndugu zetu Waislamu wanaofunga ili tuweze kufungua kula pamoja na wakati huo huo kukuza biashara za kina mama,” akasema Bw Mbogo.

Baadhi ya wafanyabiashara hao kama vile Bi Khadija Khamisi anayeuza kaimati na bajia, hakuficha tabasamu yake.

“Tangu mwezi mtukufu wa Ramadhani uanze nimekuwa nikichelewa kumaliza kuuza vyakula vyangu na wakati mwingine kurudi navyo lakini nashukuru leo nimemaliza mapema na kuangukia faida nzuri,” akasema Bi Khadija.

Kauli sawia na hiyo iliradidiwa na Bi Zulekha Omar, mchuuzi wa mahamri na viazi karai ambaye vyakula vyake vyote vilinunuliwa.

“Ninategemea biashara yangu kulea wanangu na kuwalipia karo, namshukuru kwani leo angalau nimeweza kumaliza bidhaa na kupata faida nono,” akasema.

Kwa upande mwingine vijana kwa wazee waliojumuika kwa chakula cha jioni walimshukuru Bw Mbogo kwa kuwanunulia chakula.