Habari Mseto

Ramadhani yaanza bila sherehe za kawaida

April 25th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

WAUMINI wa dini ya Kiislamu kote nchini, wanatarajia kuanza mfungo wa mwezi wa Ramadhani leo Jumamosi bila shamrashamra ambazo hushuhudiwa wakati wa mwezi huo mtukufu.

Kwa kawaida, waumini wangekongamana katika misikiti na viwanja mbalimbali nchini kwa sala maalumu ya kuadhimisha mwanzo wa Ramadhan.

Lakini hilo halitawezekana mwaka huu kwa sababu ya masharti makali yaliyowekwa kuzuia uenezaji wa virusi vya corona.

Miongoni mwa masharti hayo ni kama vile kuzuia watu kutangamana, ambayo ilisababisha misikiti na makanisa kufungwa.

Wakati wa mwezi wa Ramadhani, Waislamu hutekeleza ibada nyingi wakati wa usiku ikiwemo swala ya taraweh ambayo huswaliwa baada ya swala ya Ishaa.

Kwa sababu ya marufuku iliyowekwa, waumini hawataweza kutekeleza swala hizo za usiku.

Mwaka huu, waumini pia hawataweza kukusanyika eneo moja kwa Iftar jinsi walivyozoea.

Hii ni pamoja na Iftar ambazo huandaliwa na wafadhili mbalimbali kwa minajili ya kusaidia watu wasiojiweza katika jamii.

Kadhi Mkuu Sheikh Ahmed Muhdhar, ambaye alitangaza kuanza kwa funga ya mwezi huu siku ya leo, alisema kuna haja ya Waislamu kufuata maagizo ya serikali wakati wa Ramadhani mwezi huu.

Sheikh Muhdhar aliwaonya waumini kutotangamana kwa ajili ya ibada, kula ama kwa maombi yoyote yale kama ilivyo ada ya mwezi huu mtukufu.

“Naomba tufuate maagizo yaliyotolewa na serikali. Licha ya kuwa huu ni mwezi wa ibada, ni lazima tutambue kuwa tuko na janga ambalo linatukabili kama nchi,” akasema Sheikh Muhdhar.

Sababu ya kuanza kufunga Jumamosi

Alisema kuwa Waislamu nchini Kenya wataanza kufunga leo Jumamosi kwa sababu mwezi haukuonekana siku ya Alhamisi kama ilivyotarajiwa.

Hivyo basi jana aliambia waumini wakamilishe mwezi wa Shaaban ili waanze mwezi wa Ramadhan leo Jumamosi.

“Tumepiga simu maeneo tofauti ikiwemo Tanzania na Zanzibar na hakuna ripoti za kuonekana kwa mwezi. Hivyo basi tutaanza kufunga Jumamosi,” akasema.

Mnamo Jumatano Rais Uhuru Kenyatta aliwahimiza waumini wa dini hiyo kufuata maagizo ili kuepuka kusambaza virusi vya corona.

Baadhi ya waumini walikuwa wamemtaka Rais Kenyatta kusongeza marufuku hiyo ili kuruhusu ibada ziendelee na maskini kupata fursa ya kupokea chakula wakati wa usiku.