HabariSiasa

Ramadhani yamgeuza Joho kuwa mhubiri

May 19th, 2019 2 min read

WINNIE ATIENO na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amejulikana kwa ujasiri wake wa kisiasa na kupambana na yoyote yule ambaye angethubutu kupambana naye.

Hata hivyo, katika mwezi huu wa Ramadhani, gavana huyo ameonekana kuwa na mwenendo tofauti mbali na ule uliozoeleka kumhusu.

Bw Joho ameonekana kuwa mtulivu akitumia muda mwingi kuhubiri utangamano kati ya jamii zote nchini, umuhimu wa kuomba, kupendana na kufuata nguzo za dini ya Uislamu.

Ramadhan ni mwezi mtukufu katika kalenda ya Kiislamu ambapo jamii hiyo inatakiwa kumtumikia Mungu kwa kufunga na kuongeza kuomba mwezi mzima.

Wengi wanapomwona gavana huyo wanadhani anatazamia kuwa mhubiri kwani kila anapochukua kipaza sauti anahubiri injili ya amani, upendo na umoja kinyume na hulka yake ya kauli kali za siasa alizokuwa akichemsha.

“Lazima tuungane kama jamii, tuishi kwa amani, tuache chuki na tuanze kupendana. Uislamu unatueleza kuwa tuko sawa sote. Waislamu ni ndugu lakini kwa jamii zengine sote tuko sawa,” alisema Bw Joho hivi majuzi alipokutana na viongozi wa dini.

Aliwataka waislamu waishi maisha mema ili jamii zingine zipendezwe na Uislamu na kuvutiwa kwenye dini hiyo.

“Tukiishi kwa chuki tutafanya wengine washangae kuhusu Uislamu lakini tukiishi kwa wema watapendezwa na dini yetu,” alisema.

Amekuwa akijumuika na wakazi, vijana na viongozi wa dini kauli yake ikiwa upendo, umoja na utangamano wa jamaii zote.

Anapoulizwa na wakazi maswala ya siasa anasema hatozungumzia swala hilo hadi amalize Ramadhan.

“Kuna wakati wa siasa na utakuja lakini sasa ni wakati wa Ramadhan ambapo tunamtumikia Mungu, ni mwezi wa mapenzi, kutoa sadaka, kusaidia wasiojiweza na kuombeana. Tutaongea kuhusu siasa wakati wake lakini mwezi huu Mtukufu huwa hata nazima simu yangu sababu sitaki kukosa baraka,” alisema.

Aliwataka waislamu kusimama wima katika dini na wasiyumbishwe na mawimbi yoyote huku wakimwomba Mungu.

Ni mwezi wa Ramadhan ambapo Bw Joho anakuwa ‘mtakatifu’ akiweka dini mbele kushinda chochote kile. Lakini wale ambao wameona video za Bw Joho akiongea kuhusu kunyenyekea na kumwomba Mungu mwezi huu wanamkejeli wakisema anaazimia kuwa mhubiri.

Gavana Joho alisema kwa lolote lile ni sharti binadamu amweke Mungu mbele ili afanikiwe akisisitiza kuwa uongozi una majukumu magumu.

“Lakini tuwe na imani katika safari hii, muhimu ni kwamba tushirikiane, kuna nchi ambazo waislamu ni wachache lakini wana ushawishi mkubwa serikalini kwa mfano Afrika Kusini, humu nchini tunaweza kupata ushindi lakini lazima tujipange,” alisisitiza.

Pia aliwataka waislamu wasamaheane ili wapate baraka kutoka kwa Mungu.

Bw Joho anatarajiwa kumkaribisha Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa iftar hii leo. Wengi wanasubiri kuona kama Bw Joho atazungumzia siasa.

Iftar hiyo itafanywa katika uwanja wa shule ya msingi ya Serani.

Tayari uwanja huo umeanza kupambwa.