Ramaphosa aomba utulivu wafuasi wa Zuma wakizua fujo

Ramaphosa aomba utulivu wafuasi wa Zuma wakizua fujo

Na XINHUA

KWAZULU-NATAL, Afrika Kusini

RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa wito kuwe na utulivu nchini humo baada ya wafuasi wa Rais wa zamani Jacob Zuma kuanza maandamano makubwa ya kupinga kufungwa kwake gerezani.

Maandamano hayo yalianza mnamo Ijumaa, siku moja tu baada ya Rais huyo wa zamani kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 baada ya kupuuza amri ya mahakama ya kikatiba iliyomtaka atoe ushahidi kuhusu kesi ya ubadhirifu wa mali ya umma akiwa uongozini.

Zuma alishiriki tu kikao kimoja cha kesi hiyo mnamo Disemba mwaka jana kisha kupuuza vikao vingine vilivyoandaliwa Februari na kusababisha apokezwe adhabu hiyo kwa kudharau korti.

Mnamo Ijumaa wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani waliwasha moto na kuyachoma magurudumu ya gari na pia kuteketeza malori yanayosafirisha bidhaa katika barabara za N3, N2 na M7 kati ya barabara nyingine maarufu.

Pia ghasia na makabiliano ya polisi yalishuhudiwa maeneo mengine ya KwaZulu-Natal ambako ni ngome ya kisiasa ya Zuma.

Waandamanaji hao wanataka Zuma aachiliwe huru huku wakisema uamuzi wa kumfunga kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79 haukufikiwa kwa haki.

Hata hivyo, Rais Ramaphosa ametoa wito kwa amani akisema kufungwa kwa Zuma hakufai kutumiwe kueneza ghasia na uharibifu wa mali, hali inayovuruga utilivu ambao umekuwa nchini humo kwa miaka mingi.

“Rais Ramaphosa anasema kwamba ghasia zinazolenga kuharibu miundomsingi na barabara ambazo zimekuwa zikitumika kiuchumi, zitaishia kuathiri tu maisha ya wanayoshiriki vurugu hizo. Sababu zinazochochea ghasia hizo katika KwaZulu-Natal hazitoshi kuunga uharibifu wa mali ya umma,” akasema Kaimu Msemaji katika afisi ya Rais Tyrone Seale.

Polisi nchini Afrika Kusini tayari wamewatia mbaroni zaidi ya watu 25 ambao walishiriki maandamano ya Ijumaa na kuchoma zaidi ya malori 25 kwenye eneo la KwaZulu-Natal.

Wakfu wa Jacob Zuma umekataa kukemea maandamano hayo huku msemaji wake akisema tu ghadhabu za raia zinatokana na uamuzi wa kibaguzi wa korti.

Hapo Jumapili, msemaji wa polisi katika eneo la KwaZulu-Natal Jay Naicker alisema wameimarisha usalama katika eneo hilo na akawaonya waandamanaji dhidi ya kushiriki uharibifu wa mali ya serikali au ya watu binafsi.

“Tayari watu wengi wamekamatwa kutokana na ghasia zilizotokea wakati wa maandamano mnamo Ijumaa na wengine bado wanasakwa. Pia baadhi ya raia wanatumia maandamano hayo kupora mali ya watu binafsi katika maduka na biashara nyingine,” akasema Naicker.

You can share this post!

Wawili wafariki mamia wakikesha nje baada ya nyumba...

TAHARIRI: Elimu si jukumu la serikali pekee