Kimataifa

Ramaphosa atimua mawaziri waliokuwa wandani wa Zuma

February 28th, 2018 2 min read

Na MASHIRIKA

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

KIONGOZI mpya wa Afrika Kusini Rais Cyril Ramaphosa, ametimua mawaziri waliokuwa wandani wa mtangulizi wake Jacob Zuma.

Rais Ramaphosa, hata hivyo, alimteua mke wa zamani wa Jacob Zuma ambaye pia alikuwa mshindani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha uongozi wa chama cha National African Congress (ANC), Nkosazana Dlamini-Zuma.

Bi Dlamini-Zuma aliteuliwa kuwa waziri katika afisi ya rais.

Ramaphosa aliibuka mshindi na kuteuliwa kuwa kiongozi wa ANC baada ya kumbwaga Bi Dlamini-Zuma kwa kura chache katika uchaguzi uliofanyika Desemba, mwaka jana.

Kiongozi huyo aliyechukua hatamu za uongozi siku 12 zilizopita pia alimteua tena Nhlanhla Nene mbaye alikuwa ametimuliwa na Rais Zuma. Nene aliteuliwa kuwa waziri wa fedha.

Nene alitimuliwa na Zuma mnamo Desemba 2015, na nafasi yake ikachukuliwa na mbunge ambaye hakuwa na umaarufu. Uteuzi wa mbunge huyo ulizua joto la kisiasa hivyo kumlazimu Zuma kuteua Pravin Gordhan kutwaa wadhifa huo, siku nne baadaye.

Mkuu wa mkoa wa Mpumalanga David Mabuza aliteuliwa kuwa naibu wa rais. Bw Mabuzza pia ni naibu mwenyekiti wa chama cha ANC. Bw Zuma ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika na ufisadi alilazimishwa kustaafu na uongozi wa chama cha ANC mapema mwezi huu.

Bw Ramaphosa alichukua hatamu za uongozi huku akiahidi kukabiliana na ufisadi.

Miongoni mwa mawaziri wa Zuma waliotimuliwa ni Faith Muthambi, Mosebenzi Zwane, Des van Rooyen, David Mahlobo, Lynne Brown na Bongani Bongo.

 

Shaka

Viongozi wa Upinzani, hata hivyo, walikosoa baraza jipya la mawaziri la Rais Ramaphosa huku wakisema kuwa bado lilikuwa limesheheni mawaziri ambao maadili yao yanatiliwa shaka.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), Mmusi Maimane baadhi ya mawaziri waliosalia katika baraza walikuwa wandani wa Bw Zuma na familia ya Gupta ambayo inadaiwa kujipatia kandarasi serikalini kutokana na ushawishi wake kwa utawala wa Zuma.

Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) chake Julius Malema kilipuuzilia mbali baraza hilo huku kikisema kuwa limesheheni wafisadi walionufaika na mali ya wizi wakati wa utawala wa Zuma.

“Bathabile Dlamini ameteuliwa kuwa waziri licha ya kuandamwa na sakata za ufisadi. Dlamini nusura asambaratishe hazina ya kuwasaidia maskini allipokuwa waziri wa Maendeleo ya Kijamii,” akasema Bw Malema.