Kimataifa

Rambo achunguzwa kwa dhuluma za ngono

June 15th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa filamu Sylvester Stallone almaarufu Rambo huenda akashtakiwa hivi karibuni kwa dhuluma za ngono.

Kwa mujibu wa tovuti ya Punch nchini Nigeria, Rambo anachunguzwa na Waendesha mashtaka nchini Marekani kubaini kama anastahili kushtakiwa kwa madai ya dhuluma hizo yaliyoripotiwa mwaka 2017.

Tovuti hiyo imeripoti kwamba msemaji kutoka ofisi ya sheria ya Los Angeles, Greg Risling ametangaza kwamba idara ya polisi ya Santa Monica imewasilisha kesi dhidi ya staa huyu.

“Kesi hii inaangaliwa na jopo letu linaloshughulikia uhalifu wa dhuluma za kimapenzi.”

Kesi hiyo inahusu mwanamke mmoja aliyeripoti Novemba mwaka 2017 kwamba muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 71, ambaye anafahamika kwa kwa filamu za “Rocky” na “Rambo”, alimdhulumu mwaka 1990.

Risling alikataa kutoa habari zaidi kuhusu madai hayo ama kufafanua iwapo sheria inayozuia kushtakiwa kwa mhalifu ripoti ya dhuluma ikifanywa miaka ya miaka 10, inatumika katika kesi hii.

Polisi mjini Santa Monica pamoja na wakili wa Stallone, Martin Singer, hawakupatikana kutoa maoni yao.

Madai dhidi ya Rambo yanawasilishwa wakati kampeni ya #MeToo inayomulika dhuluma za kimapenzi katika eneo maarufu la filamu Hollywood na kwingineko, inapamba moto.

Kulingana na Singer, Rambo anapinga madai hayo, ingawa anakubali waliwahi kuna uhusiano na mwanamke huyo wakiunda filamu moja nchini Israel mwaka 1987 akiwa kapera.