Michezo

Ramos akiri kuteswa na penzi la kale, sasa halali

January 28th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya kuwa Sergio Ramos amefunga pingu za maisha na kichuna Pillar Rubio ambaye amemzalia watoto watatu, nahodha huyo wa Uhispania na Real Madrid amepania kuwasha upya mwenge wa mapenzi na aliyekuwa mchumba wake, Elisabeth Reyes, 32.

Elisabeth ambaye aliibuka mshindi wa Miss Spain mnamo 2006, kwa sasa ni mwanamitindo maarufu nchini Uhispania na mama wa mtoto mmoja.

Kipusa huyo ambaye pia amewahi kutoka kimapenzi na mwanasoka Alexis Ruano, alikula yamini ya ndoa na kiungo matata wa Cadiz, Sergio Sanchez mnamo 2014 baada ya kuchumbiana kwa miaka miwili.

Baada ya Elisabeth kutawazwa malkia wa Uhispania, Ramos alianza kulitalii buyu la asali ya kipusa huyo mnamo 2007 kabla ya kumtema miezi tisa baadaye.

Akihojiwa na gazeti la The Sun wiki jana, Ramos alikiri kuteswa na penzi la zamani la Elisabeth baada ya kichuna huyo kupasua mbarika na kufichua nyingi za jumbe ambazo beki huyo amekuwa akimtumia kupitia mitandao ya kijamii.

Ramos anashikisha kasi mipango ya kumvisha Elisabeth pete ya uchumba miezi miwili baada ya kidosho Abby Elinsky wa Marekani kukiri kwamba anateswa na penzi la beki huyo anayewindwa pia na mshindi wa zamani wa Miss BumBum, Suzy Cortez.

Abby mwenye umri wa miaka 23 ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Northern Carolina na ana historia ndefu ya kujilegeza kimapenzi kwa wanasoka maarufu kwa nia ya kuwatia kishawishini bila ya mahusiano yake ya siri kufichuka kwa wepesi.

Ramos, 32, alimfanya Pilar, 40, kuwa wake wa halali mwishoni mwa mwaka jana siku tatu baada ya kumposa kichuna huyo ambaye amekuwa akimfungulia mzinga wa asali tangu 2012.

Pilar ambaye ni mwanamitindo wa zamani, anajivunia mataji mengi ya haiba kubwa katika majukwaa mbalimbali ya kutuzwa kwa wanahabari bora nchini Uhispania. Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, amekuwa mwendeshaji wa kipindi cha ucheshi, ‘El Hormiguero’ katika kituo cha Spanish TV.

Kwa pamoja na Ramos, wamejaliwa watoto watatu wa kiume: Sergio aliyezaliwa mnamo Mei 2014, Marco mwenye umri wa miaka miwili na Alejandro ambaye alizaliwa mwanzoni mwa Machi 2018.