Habari Mseto

Range Rover zilizoibwa Uingereza kurejeshwa

April 25th, 2019 1 min read

Na ANTHONY KITIMO

BALOZI wa Uingereza Nchini, Bw Nic Hailey, ameagiza magari tisa yaliyoibwa na kusafirishwa nchini kupitia Bandari ya Mombasa, kurejeshwe Uingereza.

Bw Hailey alisema hayo baada ya kushuhudia kufunguliwa kwa kontena zilizotumika kusafirisha magari hayo ya kifahari kutoka Ulaya hadi Bandari ya Mombasa,akiandamana na maafisa wa Mamlaka ya Ushuru (KRA).

Balozi huyo alitaka magari hayo yarejeshwe Uingereza kule ambako visa hivyo vya wizi vimeripotiwa.

Pia walionya maajenti ghushi kusitisha biashara hiyo haramu.

Baadhi ya magari yaliyonaswa ni sita aina ya Range Rover, Land Cruiser Discovery moja, lingine la BMW na pia Matic.

Bw Hailey alisema biashara hiyo haramu inahusisha watu maarufu na serikali yake inashirikiana na polisi kutoka nchi mbalimbali kuwasaka washukiwa.

“Magari hayo yamepitia nchi nyingi na watu mbalimbali wamehusika. Tunaendeleza uchunguzi wetu ili kuhakikisha washukiwa wametiwa mbaroni licha ya magari haya kurejeshwa nchini Uingereza,” alisema Bw Hailey.

Alisema kufika kwao bandarini Mombasa ni onyo kali kwa wanaopanga biashara hiyo haramu.

Afisa wa KRA, Bw Githii Mburu, alisema shehena hizo ziliagizwa kama bidhaa za nyumbani na zingine kama magari madogo.

“Tulikuwa na habari za ujasusi kuhusiana na shehena hizi na tukazishikilia tukingoja wenye kuagiza lakini hatujawaona. Wezi hao walitumia stakabadhi bandia kuagiza magari hayo lakini tunaendelea na uchunguzi huo,” alisema Bw Mburu.

KRA imethibitisha gari moja la Range Rover, liliripotiwa kuibwa eneo la Oxford mjini Uingereza na wanaendelea na uchunguzi kubaini sehemu ambazo magari mengine yaliibwa.

Magari hayo yanatarajiwa kurudishwa Uingereza mwezi ujao baada ya stakabadhi muhimu kujazwa na serikali ya Kenya na ile ya Uingereza.