Michezo

Rangers, Tusker na Homeboyz zavuna pointi tatu

May 9th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Posta Rangers waliandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Ulinzi Stars katika mechi ya ligi kuu ya SportPesa iliyochezewa Afraha Stadium, Alhamisi.

Bao hilo muhimu lilipachikwa wavuni na Gerson Likono dakika ya 62, licha ya Ulinzi kutawala mchezo huo katika vipindi vyote.

Kwingineko, Tusker iliicharaza Mount Kenya United 4-1 katika mechi iliyochezewa Kenyatta Stadium, Machakos.

Mount Kenya walitangulia kuona lango dakika ya 13 kupitia kwa Amani Kyata kutokana na mkwaju wa penalti.

Mabao ya washindi yalipatikana kupitia kwa Timothy Otieno, Michael Madoya (2) na David Majak.

Mjini Bungoma, mabao mawili ya David Odhiambo na Allan Wanga katika kipindi cha kwanza yaliiwezesha Kakamega Homeboyz kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Nzoia Sugar.

Odhiambo alitangulia kuona lango la wenyeji dakika ya 13 kabla ya Wanga kuongeza la pili dakika ya 34, likiwa la 17 msimu huu na kurejea kileleni mwa orodha ya ufungaji mabao mbele ya Umar Kasumba wa Sofapaka anayejivunia mabao 16.

“Sijaamua ni mabao mangapi nalenga kufunga lakini kila nitakapopata nafasi ya kufunga, nitafunga ili niongeze idadi yangu niwezavyo msimu huu,” alisema Wanga baada ya mechi hiyo kumalizika katika uwanja wa Sudi Stadium, Bungoma.

Kocha wa Nzoia Sugar, Godfrey “Solo” Oduor alisema vijana wake walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao na kushindwa kwenye mechi hiyo ambayo sasa imeaacha katika nafasi ya 12 kutokana na pointi 32.

“Kwa jumla nilifurahia walivyocheza, ingawa hatukuwa na bahati ya kufunga mabao ya kutuwezesha kupanda hadi nafasi ya 11 kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya mechi ijayo ugenini Jumapili dhidi ya Tusker FC,” aliongeza Oduor.

Kwa upande wa Homeboyz, Nicholas Muyoti aliwapongeza vijana wake kwa ushindi huku akiwasifu kwa kupata mabao ya mapema ambayo yamewapeleka hadi nafasi ya nne kutokana na pointi 48, huku wakibakisha kucheza mechi tano.

“Tunapaswa kuendelea kusajili matokeo mem aili tutimize ndoto zetu za kumaliza katika nafasi nzuri kuliko msimu uliopita,” alisema kiungo huyo mstaa wa Harambee Stars.

Hata hivyo, mechi hiyo ilisimamishwa kwa dakika tatu kufuatia fujo za mashabiki waliolimana kabla ya maafisa wa Homeboyz kuingia uwanjani na kutuliza hali.

Baada ya maafisa wa polisi kutiliza hali hiyo, Collins Wakhungu alikaribia kumfunga bao Gabriel Andika alipoachilia kombora karibu na lango la Homeboyz.

Hansel Ochieng alikosa nafasi ya wazi dakika ya 73 minutes baada ya kuandaliwa pasi na Patrick Otieno.

Ilibidi maafisa wa polisi watumie vitoa machozi kuwatawanya mashabiki waliojazana nje ya mlango wa uwanja kushambulia mabasi mawili ya wachezaji wa Homeboyz.

Matokeo ya mechi za jana kwa ufupi ni: Sony Sugar 2 Kenyan Commercial Bank 0; Nzoia 0 Kakamega Homeboyz 2; Mount Kenya United 1 Tusker 4; Ulinzi Stars 0 Posta Rangers 1.