Michezo

Rangers yapiga marufuku wawili kwa kukiuka kanuni za kudhibiti kuenea kwa Covid-19

November 2nd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha Rangers kimewapiga marufuku kwa muda wanasoka Jordan Jones na George Edmundson kwa “kukiuka kanuni za kudhibiti msambao wa virusi vya corona”.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rangers, Jones na Edmundson walihudhuria hafla moja iliyojumuisha idadi kubwa ya watu mnamo Novemba 1, 2020 huku “kundi jingine la watu wakionekana nje ya makazi yao”.

Wawili hao kwa sasa watachunguzwa na kikosi chao na watalazimika kujitenga kwa kipindi cha siku 14 zijazo.

“Tuna kanuni zinazostahili kuongoza mienendo ya kila mmoja wetu. Hatutakubali yeyote kukiuka sheria zilizopo katika jitihada za kukabiliana na corona,” akasema mkurugenzi wa Rangers, Stewart Robertson.

“Hatua ya mchezaji wetu yeyote kuvunja kanuni zilizopo inaweka kikosi kizima katika hatari kubwa, na hili ni jambo ambalo halitakubalika kabisa,” akaongeza kinara huyo.

Rangers wameshikilia kwamba hafla iliyoandaliwa na wachezaji wao wawili hao ilifanyika saa chache baada ya kikosi hicho kusajili ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya watani wao wa tangu jadi, Kilmarnock na kufungua mwanya wa alama tisa kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Scotland.

Jones, 26, alitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Northern Ireland ambayo kocha Ian Baraclough atategemea kwenye mechi ya wiki ijayo ya kufuzu kwa fainali za Euro. Hadi alipopigwa marufuku, alikuwa amechezea Rangers mara nne pekee muhula huu.

Kwa upande wake, Edmundson, 23, amechezeshwa na Rangers mara mbili pekee hadi sasa msimu huu wa 2019-20.