Michezo

Ranieri miongoni mwa wanaomezea ukocha Guinea

September 10th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

CONAKRY, GUINEA

MKUFUNZI wa zamani wa Chelsea na Leicester City, Claudio Ranieri ni miongoni mwa makocha ambao wameorodheshwa kuwania nafasi ya kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Guinea.

Ranieri aliyewaongoza Leicester kutia kibindoni ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2016, ni kati ya wakufunzi wengine 87 waliowasilisha maombi ya kunoa Guinea, na ni kati ya wakufunzi 17 ambao wanaunga orodha ya mwisho ya wale watakaohojiwa na vinara wa Shirikisho la Soka la Guinea (Feguifoot).

Kulingana na Feguifoot, Ranieri ambaye alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), atafanyiwa mahojiano jijini Conakry mnamo Alhamisi wiki hii. Kati ya wakufunzi wote waliowasilisha maombi ya kuwania nafasi ya ukufunzi kambini mwa Guinea, ni Ranieri ndiye wa haiba kubwa zaidi.

Ranieri aliagana na kikosi cha AS Roma mnamo Mei 2019. Amewahi pia kudhibiti mikoba ya vikosi vya Juventus, Inter Milan, Atletico Madrid, Valencia na AS Monaco.

Makocha wengine ambao wanaunga orodha ya wale watakaofanyiwa mahojiano na Feguifoot ili kutoana jasho na Ranieri ni mkufunzi wa zamani wa Ubelgiji, Tunisia na Algeria Georges Leekens na Florent Ibenge aliyeagana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Kocha wa zamani wa Burkina Faso na Gabon Paulo Duarte na aliyekuwa mkufunzi wa Togo Didier Six pia ni miongoni mwa wale wanaopigiwa upatu wa kupokezwa mikoba ya Guinea.

Mwingine ni Francois Zahoui ambaye amewahi pia kuwatia makali vijana wa Ivory Coast na Niger.

Kufutwa kwa Paul Put

Guinea wanamtafuta kocha atakayelijaza pengo la Paul Put aliyepigwa kalamu mwishoni mwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizoandaliwa nchini Misri kati ya Juni na Julai 2019.

Kufutwa kwake kulichochewa na matokeo duni ya Guinea ambao walibanduliwa kwenye hatua ya 16-bora katika kivumbi hicho.

Put amewahi pia kuwatia makali vijana wa Harambee Stars kabla ya kujizulu kwake kuchochea Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kumwajiri Sebastien Migne aliyefutwa mwezi uliopita. Feguifoot imempokeza Put marufuku ya maisha ya kutojihusisha kabisa na masuala ya soka baada ya kupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu, kukiuka maadili na kanuni za shirikisho hilo.