Raphinha awabeba Brazil dhidi ya Venezuela katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia

Raphinha awabeba Brazil dhidi ya Venezuela katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

FOWADI Raphinha Belloli wa Leeds United alisaidia timu ya taifa ya Brazil kutoka nyuma na kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Venezuela mnamo Alhamisi usiku katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Raphinha alitokea benchi katika kipindi cha pili kwenye mchuano huo uliokuwa wake wa kwanza kusakata ndani ya jezi za Brazil.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alijiondoa katika kikosi cha Brazil mnamo Septemba baada ya klabu za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuzuia wachezaji kurejea katika mataifa yao kama mojawapo ya mbinu za kudhibiti msambao wa corona.

“Kocha Tite Bacchi aliniomba nifanyie Brazil mambo ambayo ninawafanyia Leeds United. Singetamani kabisa kumuangusha kocha wangu, wachezaji wenzangu au mashabiki wetu wa Brazil baada ya ombi hilo,” akasema Raphinha aliyechangia mabao mawili yaliyofungwa na timu yake ya taifa.

Brazil walijipata nyuma kwa bao 1-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza mjini Caracas baada ya Eric Ramirez kuwaweka wenyeji Venezuela kifua mbele.

Bao hilo liliwaweka Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia katika hatari ya kupoteza dhidi ya Venezuela kwa mara ya kwanza baada ya mechi 18 za kufuzu kwa fainali za kipute hicho.

Hata hivyo, Tite alimleta Raphinha katika nafasi ya William Ribeiro wa Everton mwanzoni mwa kipindi cha pili na akashirikiana vilivyo na Vinicius Jr na Antony.

Krosi ya Raphinha ilijazwa wavuni na beki Marquinhos wa Paris Saint-Germain (PSG) aliyesawazisha mambo katika dakika ya 71 kabla ya Gabriel Barbosa kufunga penalti na kuwaweka Brazil kifua mbele.

Mwishoni mwa kipindi cha pili, Raphinha alitoa krosi nyingine murua iliyokamilishwa na Antony wa Ajax.

“Nilikuwa na mchecheto mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba ilikuwa mechi yangu ya kwanza kuchezea timu ya taifa ya Brazil. Hata hivyo, nilijitahidi na kuchangia ushindi wa kikosi kizima,” akasema Raphinha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Umiliki wa Newcastle United watwaliwa na mabwanyenye wa...

Argentina na Paraguay waambulia sare tasa katika mechi ya...