Michezo

Rashford afunga mawili na kusaidia Man-United kuongeza masaibu ya Sheffield United ligini

December 18th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer alikuwa mwingi wa sifa kwa vijana wake wa Manchester United baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Sheffield United mnamo Alhamisi kuwapaisha hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mabao mawili kutoka kwa fowadi Marcus Rashford yalisaidia Man-United kuendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa ugenini kwenye ligi hadi kufikia sasa msimu huu.

Akicheza dhidi ya kikosi chake za zamani, kipa Dean Henderson, alifanya masihara katika dakika ya tano na kumpa David McGoldrick fursa ya kucheka na nyavu zake baada ya kushirikiana vilivyo na Oliver Burke.

John Fleck alipoteza nafasi maridhawa ya kufanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 15. Hata hivyo, Rashford alisawazisha mambo katika dakika ya 26 baada ya kukamilisha krosi safi aliyoandaliwa na beki Victor Lindelof aliyemtatiza pia kipa Aaron Ramsdale mwishoni mwa kipindi cha pili.

Anthony Martial alikamilisha ukame wa dakika 491 wa mabao kapuni mwake kwa kutikisa nyavu za Sheffield United baada ya kupokezwa pasi nzuri na kiungo Paul Pogba.

Bao hilo liliamsha zaidi motisha ya Man-United waliofungiwa goli la ushindi na Rashford kunako dakika ya 51.

Alama tatu zilizovunwa na Man-United ziliwawezesha kuchupa hadi nambari sita jedwalini kwa alama 23 sawa na nambari tano Everton. Ni pengo la pointi moja pekee ndilo linalowatenganisha Man-United na Leicester City wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kwa upande wao, Sheffield United wanaotiwa makali na kocha Chris Wilder bado wanavuta mkia wa jedwali kwa alama moja pekee. Mechi dhidi ya Man-United ilikuwa ya nane mfululizo kwa Sheffield United kupoteza kwenye kampeni za EPL hadi kufikia sasa msimu huu.

Ushindi wa Man-United ulishusha pakubwa presha ambayo ilianza kumvaa Solskjaer mwezi wa Novemba baada ya kikosi chake kushindwa na Arsenal ligini kisha kupepetwa na Istanbul Basaksehir kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Man-United wanatarajiwa sasa kutia fora zaidi kwenye kampeni za EPL baada ya kubanduliwa kwenye soka ya UEFA na badala yake kushuka hadi Europa League.

Licha ya kusajili ushindi wa sita mfululizo kwenye EPL ugenini msimu huu, Man-United wamejipata nyuma kwa wapinzani kutangulia kuona lango lao katika kila mojawapo ya mechi hizo.

Sheffield United kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Brighton uwanjani Amex mnamo Disemba 20 huku Man-United wakiwaalika Leeds United kwa kivumbi kingine cha EPL siku hiyo.