Dimba

Rashford hana muda mchafu, ni baibai Lucia, ingia ndani Erica

May 4th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

NYOTA wa Manchester United, Marcus Rashford, 26, amepata hifadhi mpya ya penzi lake kwa mwanamitindo mzaliwa wa Colombia, Erica Correa.

Wawili hao walionekana wiki hii wakiponda raha katika eneo la watu mashuhuri (VIP) ndani ya kilabu cha usiku cha Blvd Manchester, Uingereza.

Walinzi wa kilabu hicho waliwapeleka baadaye katika sehemu ya juu walikoburudishwa kwa muziki wa RnB hadi usiku wa manane.

Ingawa kilabu hicho kilikuwa na watu wengine maarufu, wakiwemo wanasoka wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), wadaku waliohojiwa na gazeti la The Sun walisema Rashford alitaka tu kuzungumza na Erica pekee.

“Kwa wakati fulani, wasaidizi na walinzi wake walionekana wakija karibu na wapenzi hao na kuwazingira licha ya kwamba walikuwa wakishiriki mazungumzo yao ya faragha,” akasema mdaku mmoja.

Erica alihamia Liverpool nchini Uingereza akiwa na umri wa miaka mitano pekee.

Aliwaniwa na mashirika mengi ya uanamitindo akiwa na umri wa miaka 13 na akapata fursa tele za kunogesha maonyesho ya fasheni na hafla za uvumishaji wa huduma na bidhaa za kampuni mbalimbali nchini India, Ugiriki, Italia na Amerika.

Miezi miwili iliyopita, msemaji wa familia ya Rashford alithibitisha kuwa fowadi huyo raia wa Uingereza alikuwa akisaka demu mpya baada ya kutemana rasmi na kisura Lucia Loi.

Alitengana na mchumba wake huyo wa muda mrefu baada ya kurudiana kwa kipindi kifupi mnamo Novemba. Awali, walikuwa tena wameachana mwanzoni mwa 2023 licha ya kukaa pamoja katika uhusiano wa kimapenzi kwa kipindi cha miaka 10.

Tangu atemane na Lucia, miguu ya Rashford iliingia kutu na ukame wa mabao ukamwandama katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Sasa analazimika kupigania nafasi ya kujumuishwa katika kikosi kitakachotegemewa na Uingereza kwenye fainali za Euro nchini Ujerumani mwaka huu.

Hata hivyo, mashabiki wanatumai kwamba Erica, 29, atamrejesha Rashford katika mwelekeo sahihi na kuchochea nyota yake ianze kuangaza tena.

Rashford alivisha Lucia pete ya uchumba mnamo Mei 2022 katika mkahawa wa Catch LA jijini Los Angeles, Amerika.

Kichuna huyo, ambaye ni afisa wa uhusiano mwema katika kampuni moja ya sukari nchini Uingereza, alianza kumfungulia Rashford mzinga wake wa asali mnamo 2013 wakiwa wanafunzi katika Shule ya Mersey iliyoko Ashton, Manchester.