Habari

RASMI: Githu amkabidhi Paul Kihara ofisi ya Mwanasheria Mkuu

April 3rd, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai Jumanne alimkabidhi rasmi ofisi mrithi wake Jaji Paul Kihara akisema kwamba anajivunia huduma alizotoa kwa wakenya kwa kipindi cha miaka saba aliyohudumu.

Prof Muigai ambaye ana tajriba ya miaka mingi katika taaluma uanasheria alijiuzulu mapema mwezi Februari. Katika hotuba fupi aliyotoa, aliwashukuru walioshirikiana naye na kuwataka kufanya hivyo kwa mrithi wake.

Kwa upande wake Jaji Kihara ambaye aliapishwa wiki jana katika Ikulu ya Rais alisema katiba ndiyo itakuwa ngao katika kutekeleza majukumu yake.

“Nitakumbatia katiba katika utekelezaji wa kazi zangu na nitawajibikia wakenya wote,” akasema.

Alishukuru mtangulizi wake kwa hatua ambazo taifa zimepiga tangu achukue hatamu kama mwanasheria mkuu mwaka wa 2011.

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika jumba la Sheria,  Prof Muigai alipomkabidhi ofisi Jaji Kihara kama mwanasheria mkuu mpya.

Prof Githu Muigai (kushoto) alipomkabbidhi rasmi Paul Kihara ofisi ya Mwanasheria Mkuu Aprili 3, 2018 jijini Nairobi. Picha/ Martin Mukangu

Githu aliteuliwa na kupendekezwa kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu mwezi Januari mwaka 2011 lakini uteuzi huo ulipingwa vikali na Waziri Mkuu wakati huo Raila Odinga kwa kigezo kwamba hakushauriwa na Rais Kibaki.

Aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na na Waziri Mkuu Raila Odinga walikuwa washirika kwenye iliyokuwa serikali ya muungano maarufu kama nusu mkate iliyobuniwa baada ya uchaguzi tata wa mwaka 2007.

Hata hivyo mambo yalimwendea shwari Mwezi Agosti mwaka huo Raila na Kibaki walipokubaliana na akapokezwa rasmi wadhifa huo.

Anatambuliwa mno kama moja wa waliokuwa katika mstari wa mbele kuandika rasimu ya katiba ya Bomas(Bomas draft) ambayo inatumika kwa sasa baada ya kurasmishwa mwaka 2010.

Prof Muigai alikuwa akihudumu kama mwanasheria mkuu wa tano tangu taifa lijinyakulie uhuru.

Waliokuwa watangulizi wake ni Charles Njonjo(1963-1980), James Karugu( 1981-1983), Mathews Guyu Muli(1983-1991) na Amos Wako(1991-2011) .

Aidha mrithi wake Jaji Paul Kihara si mgeni katika taaluma ya uanasheria. Kihara amehudumu kama rais wa mahakama ya rufaa tangu mwaka wa 2012 hadi kuteuliwa kwake.

Jaji huyo aliteuliwa kama mojawapo wa majaji wa mahakama kuu mwaka 2003 na pindi tu serikali Rais Mstaafu Mwai Kibaki ilipoingia mamlakani.

Baadhi ya nyadhifa alizohudumu ni Mkuu wa Taasisi ya kutoa Mafunzo kwa Majaji, Mkurugenzi wa Chuo cha Uanasheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza Utendakazi wa Majaji.