Michezo

Ratiba mpya yaChampionship yatolewa

June 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MECHI kati ya Fulham na Brentford imeratibiwa kuwa ya kwanza kusakatwa wakati kampeni za soka ya Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) itakaporejelewa mnamo Juni 20, 2020.

Gozi kati ya klabu hizo zinazopigania nafasi ya kufuzu kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litaanza saa nane na nusu mchana uwanjani Craven Cottage.

Hakuna mchuano wowote wa Championship umetandazwa tangu Machi 8, 2020 baada ya kuahirishwa kutokana na janga la corona.

Pambano lililowashuhudia Derby wakiwanyuka Blackburn 3-0 ndiyo mechi ya mwisho kusakatwa katika Championship.

Kuanza upya kwa kipute hicho kumetegemezwa kwa vikosi vyote vya Championship kuzingatia kanuni zilizopo za afya katika jitihada za kukabiliana na maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Viongozi wa jedwali la Championship, Leeds United ambao pia wanalenga kunogesha kivumbi cha EPL msimu ujao, watavaana na Cardiff City mnamo Juni 21.

West Bromwich Albion wanaoshikilia nafasi ya pili jedwalini watakwaruzana na Birmingham City katika mojawapo ya mechi 10 ambazo zimepangiwa kuanza saa kumi na moja jioni mnamo Juni 20.

Ratiba mpya kwa minajili ya michuano yote iliyosalia msimu huu katika kipute cha Championship ilitolewa na wasimamizi wa ligi hiyo mnamo Juni 8, 2020.

Hakutakuwa na mechi za katikati ya wiki ya Juni 23-24 hadi juma litalofuatia ambalo litashuhudia vikosi vyote vikikabiliana kwa matarajio ya kukamilisha msimu mnamo Julai 22, 2020.

RATIBA MPYA YA CHAMPIONSHIP:

Jumamosi Juni, 20:

Blackburn Rovers na Bristol City

Fulham na Brentford

Huddersfield Town na Wigan Athletic

Hull City na Charlton Athletic

Luton Town na Preston North End

Middlesbrough na Swansea City

Millwall na Derby County

Queens Park Rangers na Barnsley

Reading na Stoke City

Sheffield Wednesday na Nottingham Forest

West Bromwich Albion na Birmingham City

Jumapili, Juni 21:

Cardiff City na Leeds United