Ratiba ngumu kwa Juventus mnamo Januari 2021. Je, watajinyanyua?

Ratiba ngumu kwa Juventus mnamo Januari 2021. Je, watajinyanyua?

Na MASHIRIKA

JUVENTUS wanakabiliwa na kibarua kizito cha kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa mara ya 10 mfululizo ikizingatiwa ugumu wa ratiba yao katika mwezi huu wa Januari.

Chini ya kocha mpya Andrea Pirlo, Juventus walianza vibaya kampeni za muhula huu na kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 24 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na viongozi AC Milan ambao wametandaza mchuano mmoja zaidi.

Baada ya likizo fupi iliyopisha sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya, Juventus wanarejelea kampeni zao za Serie A mnamo Januari 3 kwa mchuano dhidi ya Udinese.

Kukamilika kwa mechi hiyo kutawafungulia ratiba ngumu ya kuvaana na vikosi vitatu vinavyodhibiti kilele cha jedwali la Serie A huku wakitarajiwa pia kunogesha vipute vya Italian Cup na SuperCup.

Vikodi viwili vya Milan ambavyo ndivyo vya pekee baada ya Juventus kuwahi kutwaa taji la Serie A chini ya kipindi cha miaka 20 iliyopita, vimeanika ukubwa wa maazimio ya kutia kapuni ufalme wa Ligi Kuu ya Italia muhula huu.

AC Milan kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Serie A kwa alama 34, moja pekee mbele ya Inter Milan wanaotiwa makali na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte.

AS Roma wanafunga mduara wa tatu-bora kwa alama 27, moja mbele ya nambari nne Sassuolo.

Baada ya kupepetana na Udinese, Juventus watawazuru AC Milan ugani San Siro mnamo Januari 6 kabla ya kuwa wenyeji wa Sassuolo jijini Turin kisha kuwaendea Inter Milan ugani San Siro.

Licha ya kukamilisha kampeni zao za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wakiwa kileleni mwa kundi, Juventus wamekuwa wakisuasua huku wakijipata mara nyingine katika ulazima wa kumtegemea sana fowadi matata raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo.

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid amewafungia Juventus jumla ya mabao 12 kutokana na 25 yanayojivuniwa na waajiri wake hadi

Katika ligi, Juventus wameambulia sare mara sita na kushinda mechi sita kutokana na 13 zilizopita. Mchuano wa pekee ambao wamepoteza ni ule uliowashuhudia wakipigwa 3-0 na Fiorentina ugenini kabla ya Krismasi.

“Mara nyingine hutokea katika soka. Hatuko katika asilimia 100 ya ubora wetu. Itatulazimu kujinyayua punde na kuanza kushinda mechi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa taji la Serie A kwa mara ya 10 mfululizo,” akasema Pirlo aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Maurizio Sarri mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

Tumaini kubwa zaidi kwa Pirlo hata hivyo ni kwamba Juventus waliwahi kujipata katika nafasi ya 12 baada ya mechi 10 za ufunguzi wa msimu wa 2015-16 kabla ya kujinyanyua na hatimaye kutwaa ubingwa wa taji la Serie A.

Chini ya kocha Stefano Pioli, AC Milan wameratibia kuvaana kesho Jumapili na Benevento huku Inter Milan wakiwaalika Crotone. AC Milan watakosa huduma za fowadi Zlatan Ibrahimovic katika mchuano was aba mfululizo ligini baada ya sogora huyo raia wa Uswidi kupata jeraha la goti.

Roma watakuwa wenyeji wa Sampdoria ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama 17, tano nyuma ya nambari saba Atalanta ambao watawaalika Sassuolo.

Nambari tano Napoli watalenga kufuta rekodi mbovu ya kutosajili ushindi katika jumla ya mechi tatu mfululizo watakapowaendea Cagliari japo watakosa maarifa ya mfumaji Dries Mertens, beki Kalidou Koulibaly na mshambuliaji chipukizi raia wa Nigeria, Victor Osimhen anayeuguza jeraha la bega.

TAKWIMU MUHIMU KATIKA SERIE A:

26 – Alama za Sassuolo baada ya mechi 14.

12 – Mabao ya Cristiano Ronaldo anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa Serie A hadi sasa msimu huu.

7 – Idadi ya mechi ambazo Inter Milan wameshinda kwa mfululizo ligini.

3 – Idadi ya mechi ambazo zimesakatwa na Napoli bila ushindi.

2 – Miezi ambayo Cagliari wamekamilisha bila ya kusajili ushindi ligini

1 – Pengo la alama linalotenganisha AC Milan na Inter Milan kileleni mwa jedwali la ligi.

RATIBA YA SERIE A (Januari 3, 2021):

Inter Milan na Crotone

Atalanta na Sassuolo

Cagliari na Napoli

Fiorentina na Bologna

Genoa na Lazio

Parma na Torino

AS Roma na Sampdoria

Spezia na Hellas Verona

Benevento na AC Milan

Juventus na Udinese

You can share this post!

Waithera: Krismasi ya 2020 ni ya kwanza kuadhimishia...

CHOCHEO: Kupata mchumba si muujiza, lazima utoke ukutane na...