Michezo

Ratiba ya mechi za Jumapili za ligi kuu ya Super 8

March 16th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MICHUANO ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Super 8 itaendelea Jumapili katika viwanja mbalimbali, huku waliokuwa mabingwa, Kawangware United wakivaana na majirani Meltah Kabiria FC ugani Riruta BP Stadium.

Timu zote zinajivunia wafuasi wengi wanaotarajiwa kufurika uwanjani humo kushuhudia pambano hilo la ‘Dagoretti Derby’ .

Chini ya ukufunzi wa Francis Thairu, Kawangware ambao walianza vibaya kampeni zao kwa kushindwa 3-0 na Lebanon wanatarajiwa kucheza kwa makini ili kuepuke kichapo kingine.

Vijana hao ambao walimaliza katika nafasi ta tano mwaka uliopita, walishindwa 1-0 na Kaberia katika mechi ya marudiano baada ya sare ya 0-0 katika mkondo wa kwanza, msimu uliopita.

“Itakuwa mechi ngumu, lakini sisi kama wenyeji tunatoa mwito kwa mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kushangilia vijana ili wafanye vizuri,” alisema Thairu.

Kabiria ambao walimaliza katika nafasai ya tisa msimu uliopita, walinza mwaka huu kwa kulimwa 3-1 na mabingwa watetezi Jericho All-Stars wanakamata nafasi ya 14 jedwalini kwenye ligi hiyo inayojumuisha timu 16.

Kwingineko, Lebanon FC watakuwa ugenini kupepetana na Rongai All-Stars katika uwanja wa shule ya Nakeel.

TUK FC wataikaribisha Team Umeme katika uwanja wa Kabete Cavs baada ya kushindwa 1-2 na  Rongai.

Baada ya kipigo cha ghafla cha 1-0 kutoka kwa Shauri Moyo Sportiff, Makadara Junior League SC ambao walimaliza katika nafasi ya tatu watakabiliana na Githurai All-Stars.

Mathare Flames, zamani Zamalek FC watakutana na Dagoretti Former Players FC ugani Drive Inn wakati Huruma Kona wakiikaribisha Metro Sports mtaani Huruma.

Ratiba ya mechi za Jumapili ni:

Meltah Kabiria na Kawangware United (Riruta BP Stadium, saa tisa); Makadara Junior League SA na Githurai All Stars (Hamza grounds, saa tisa); TUK na Team Umeme (Kabete Cavs, saa tisa); Shauri Moyo Sportif na NYSA (Makongeni, saa tisa); Rongai All Stars na Lebanon FC (Nakee, saa tisa); Mathare Flames na Dagoretti Former Players FC (Drive Inn, saa tisa); Huruma Kona na Metro Sports FC (Huruma, saa tisa).