Michezo

Ratiba ya Prinsloo Sevens yatolewa

July 16th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MAKUNDI ya duru ya ufunguzi ya raga ya kitaifa ya wachezaji saba kila upande ya Prinsloo Sevens, yametangazwa.

Mabingwa wa mwaka 2017 Kabras Sugar wameratibiwa kuanza kutetea taji la kitaifa dhidi ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo Julai 21 mjini Nakuru.

Kabras wako katika Kundi A pamoja na Strathmore Leos, Mwamba na Mean Machine.

Mabingwa wa Kenya mwaka 2016 Homeboyz wametiwa katika Kundi B pamoja na Kenya Harlequin, Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na Kisumu.

Kundi C linaleta pamoja Impala Saracens, Menengai Oilers, Western Bulls na Mombasa.

Mabingwa wa Prinsloo Sevens mwaka 2017 KCB wako katika Kundi D pamoja na wenyeji Nakuru na Nondescripts na Nzoia Sugar Webuye.

Raga za mwaka 2018 zimedhaminiwa na benki ya Stanbic, ambayo pia inafadhili klabu ya Mwamba.

Ratiba ya Raga ya Kitaifa mwaka 2018

Julai 21-22: Prinsloo Sevens (Nakuru Athletic Club)

Julai 28-29: Sepetuka Sevens (Eldoret Sports Club)

Agosti 18-19: Kabeberi Sevens (Machakos)

Agosti 25-26: Driftwood Sevens (Mombasa Sports Club)

Septemba 8-9: Dala Sevens (Mamboleo Showground Kisumu)

Septemba 15-16: Christie Sevens (RFUEA Ground Nairobi)