Habari za Kitaifa

Raychelle Omamo na Faith Odhiambo: Wanawake pekee kuwaongoza mawakili nchini

March 1st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

USHINDI wa Bi Faith Mony Odhiambo kama kiongozi mpya wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK), umetajwa kuwa wa kipekee, kwani ndiye mwanamke wa pili kukiongoza chama hicho baada ya Bi Raychelle Omamo.

Bi Omamo ndiye alikuwa mwanamke wa kwanza kukiongoza chama hicho kati ya 2001 na 2003.

Bi Odhiambo alitangazwa mshindi kufuatia uchaguzi uliofanyika Alhamisi. Amekuwa akihudumu kama naibu kiongozi wa Bw Eric Theuri, ambaye ndiye kiongozi anayeondoka wa chama hicho.

Atakuwa kiongozi wa 51 wa chama hicho.

Bi Otieno alikuwa na washindani watano wakuu, ambao ni: Bw Peter Wanyama, Bi Carolyne Kamende, Bi Harriet Mboche na Bw Kipkoech Bernhard Ngetich.

Muhula wa Bw Theuri utakamilika Machi 25, 2024. Nafasi hiyo ilitangazwa kuwa wazi mnamo Desemba 5, 2023, kulingana na kanuni za chama hicho za 2020.

Kufuatia ushindi wake, mpinzani wake wa karibu, Bw Peter Wanyama, alikubali kushindwa.

Kwenye taarifa mara tu baada ya uchaguzi huo, Bw Wanyama alihusisha kushindwa kwake na dhana zilizoenezwa kwamba alikuwa akifadhiliwa na serikali.

“Hilo liliathiri sana kampeni zangu kwa wakati huo wote. Sikupokea hata senti moja kutoka kwa serikali. Nimefanya kesi nyingi dhidi ya serikali ya kitaifa,” akasema.

Je, unamfahamu Bi Omamo kwa undani, ambaye ndiye mwanamke wa kwanza kukiongoza chama hicho?

Pia, alihudumu kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni na baadaye Ulinzi katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Bi Omamo alizaliwa mnamo Julai 1962, na alikuwa mwanawe waziri wa zamani, marehemu William Omamo.

Yeye ni wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya. Alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Kent, Canterbury, Uingereza.

Alihudumu kama Wakili wa Kiwango cha Juu (SC) na Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya kwa jumla ya miaka 27.

Kabla ya kuchaguliwa kama kiongozi wa chama hicho mnamo 2001, alikuwa amehudumu kama mwanachama wa bodi yake kati ya 1996 na 2000.

Pia, amehudumu katika mataifa tofauti kama balozi wa Kenya. Baadhi ya mataifa hayo ni Ufaransa na Ureno.

Zaidi ya hayo, alikuwa mwanachama wa jopo iliyopendekeza kubuniwa kwa Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC).