Michezo

RB Leipzig wazamisha Mainz 05 nayo matokeo duni ya Schalke 04 yakimning'iniza kocha pembamba zaidi

May 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Timo Werner, 24, alifunga mabao yake ya kwanza tangu kurejelewa kwa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya miezi miwili kutokana na janga la corona.

Magoli matatu ya nyota huyo anayehemewa pakubwa na Liverpool yalisaidia RB Leipzig kuwapepeta Mainz 5-0 na hivyo kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali.

Kwingineko, Augsburg walimzidishia kocha Dvid Wagner presha na kuning’iniza padogo matumaini yake ya kuendelea kudhibiti mikoba ya Schalke waliopokezwa kichapo cha 3-0.

Schalke kwa sasa hawajasajili ushindi wowote katika jumla ya mechi tisa zilizopita, na wamefunga mabao mawili pekee kutokana na michuano hiyo.

Fortuna Dusseldorf ambao pia wananing’inia pembamba mkiani mwa jedwali walipokonywa alama tatu muhimu mwishoni mwa dakika za mwisho baada ya utepetevu wao kuwaruhusu Cologne kutoka chini kwa mabao 2-0 na kulazimisha sare ya 2-2.

Licha ya kupoteza mchuano mmoja pekee kati ya minane iliyopita, kikosi cha Fortuna kinachonolewa na Uwe Rosler kimo katika orodha ya klabu tatu za mwisho kwa alama tatu zaidi nje ya mduara wa timu zitakazoshushwa daraja mwishoni mwa muhimu huu.

Werner alifunga mabao matatu na kuchangia mengine matatu mnamo Novemba 2019 wakati ambapo Leipzig waliwapepeta Mainz 8-0. Ushindi huo ndio mnono zaidi kuwahi kusajiliwa na Leipzig katika historia yao ya kushiriki kivumbi cha Bundesliga.

Werner alijibwaga ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Mainz alitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kufunga bao moja pekee kutokana na jumla ya michuano minane iliyotangulia.

Sogora huyo alihitaji dakika 11 pekee za kwanza ugani kucheka na nyavu za Mainz baada ya kushirikiana vilivyo na Konrad Laimer.

Mabao mengine ya Leipzig yalifumwa wavuni na Yussuf Poulsen na Marcel Sabitzer kabla ya Werner kufanya mambo kuwa 5-0.

Huku ushindi wa Leipzig ukiwakweza pazuri jedwalini na kuweka hai matumaini yao ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, Schalke walishuka zaidi jedwalini na kudidimiza hata matumaini finyu ya kunogesha kampeni za Europa League muhula ujao.

Kufikia Januari 17, 2020 walipowachabanga Borussia Monchengladbach 2-0, Schalke walikuwa wakishikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama nne pekee nyuma ya Bayer Leverkusen waliokuwa wakikamata nafasi ya nne.

Tangu wakati huo, Schalke wameambulia sare mara nne na kupoteza mechi tano kati ya tisa katika kipute cha Bundesliga. Kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane huku pengo la alama 24 likitamalaki kati yao na Bayern Munich wanaoselelea kileleni mwa jedwali kwa pointi 61.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumapili):

Schalke 0-3 Augsburg

Mainz 0-5 Leipzig

Cologne 2-2 Dusseldorf