Michezo

Reading FC mazungumzoni na Beijing Renhe kuongeza kandarasi ya Ayub Timbe

June 27th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Reading imeanzisha mazungumzo na waajiri wa winga Mkenya Ayub Masika Timbe kuhusu kuongeza kipindi chake cha mkopo ambacho kitakatika Juni 30.

Mbali na kuzungumza na Beijing Renhe inayoshiriki Ligi ya Daraja la Pili nchini China iliyokopesha Reading mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, Reading pia inataka kuongeza kandarasi za kiungo Muingereza Ovie Ejaria, beki Muamerika Matt Miazga, kiungo wa Guinea-Bissau Pele na mshambuliaji wa Argentina Lucas Boye wanaoichezea kwa mkopo kutoka kwa Liverpool, Chelsea, Monaco na Torino mtawalia.

Timbe, ambaye pia ana uraia wa Ubelgiji, alijiunga na Reading katika siku ya mwisho ya kipindi kifupi cha uhamisho kilichopita (Januari 31) kwa mkopo wa miezi mitano unaofikia tamati Juni 30.

Renhe na Reading zinamilikiwa na mfanyabiashara Mchina Dai Yongge.

Timbe, ambaye kandarasi yake na Renhe itatamatika Desemba 31, 2020, amechezea Reading mechi tatu.

Michuano yake miwili ya kwanza ilikuwa ligini dhidi ya Sheffield Wednesday na Barnsley.

Aliingia mechi dhidi ya Wednesday katika nafasi ya mchezaji wa timu ya taifa ya Uingereza ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21 Ejaria katika dakika ya 86 mnamo Februari 15. Katika mchuano huo, Yakou Meite, George Puscas na Sam Baldock walifunga mabao ya Reading ikilemea wenyeji Wednesday 3-0 uwanjani Hillsborough.

Alichezeshwa pia kama nguvu-mpya dhidi ya Barnsley anayochezea beki wa pembeni kushoto Mkenya-Muingereza Clarke Oduor. Alijaza nafasi ya Mfaransa-Muingereza Michael Olise katika dakika ya 71 mnamo Februari 29 huku Reading ikititiga Barnsley 2-0 uwanjani Madejski.

Mechi yake ya mwisho kabla ya janga la virusi hatari vya corona kuvuruga michezo kote duniani ilikuwa katika Kombe la FA dhidi ya Sheffield United inayoshiriki Ligi Kuu mnamo Machi 3. Reading ilipigwa 2-1 katika muda wa ziada wa mechi hiyo ya raundi ya tano ya kombe hilo uwanjani Madejski. Alikuwa pia ametumiwa kama mchezaji wa akiba akichukua nafasi ya Olise dakika ya 98.

Ripoti kutoka Reading zinasema kuwa matokeo ya mazungumzo kati ya Reading na klabu za wachezaji hao watano yatajulikana Juni 30.

Reading kwa sasa inashikilia nafasi ya 14 kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Uingereza kwa alama 49 baada ya kusakata mechi 38.

Vijana wa kocha Mark Bowen watazuru nambari 12 Derby County uwanjani iPro leo Jumamosi saa tisa alasiri.