Michezo

Reading yarefusha kandarasi ya Ayub Timbe

July 1st, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WINGA Mkenya Ayub Masika Timbe ataendelea kuwa mchezaji wa Reading FC kwa mkopo kutoka Beijing Renhe hadi mwisho wa msimu huu baada ya klabu hiyo kuongeza kandarasi yake iliyokuwa ikatike Juni 30.

Tovuti ya Reading Chronicle imesema Julai 1 kuwa kocha Mark Bowen pia amethibitisha kuongeza kandarasi za mikopo za Ovie Ejaria, Matt Miazga, Pele na Lucas Boye kutoka klabu za Liverpool, Chelsea, Monaco na Torino mtawalia.

Kandarasi ya Timbe uwanjani Madejski iliratibiwa kutamatika Juni 30 baada ya kujiunga na Reading kutoka Renhe inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili Uchina mnamo Januari 30, 2020.

Kandarasi za wachezaji hao wote watano zilipangwa kukatika Juni 30.

Hata hivyo, kuvurugwa kwa ligi hiyo na janga la virusi hatari vya corona kwa siku 100 kulisukuma Uingereza kutangaza tarehe mpya za ligi hiyo kuwa Juni 20 hadi Julai 22.

Timbe amechezeshwa na Reading dakika 31 tangu awasili. Alitumiwa kama mchezaji wa akiba dhidi ya Sheffield Wednesday mnamo Februari 15 kwa dakika nne, akapata dakika 19 dhidi ya Barnsley (Februari 29) na kuchezeshwa dakika nane dhidi ya Derby County (Juni 27).

Alikuwa kitini dhidi ya Wigan Athletic (Februari 26), Birmingham (Machi 7) na Brentford (Juni 30).

Reading inashikilia nafasi ya 16 katika ligi hiyo ya timu 24 kwa alama 49 kutokana na mechi 40 baada ya kupoteza 3-0 dhidi ya Brentford inayofukuzia tiketi ya kushiriki Ligi Kuu katika mechi yake iliyopita.

Kichapo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Reading iliyopoteza kabisa nafasi finyu iliyokuwanayo ya kufuzu kushiriki mechi za muondoano za kuingia Ligi Kuu. Reading sasa iko alama saba pekee nje ya mduara hatari wa kutemwa.