Michezo

Real haiwezi kumtimua Zidane – Mourinho

September 25th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

KOCHA wa zamani wa Chelsea na Manchester United, Jose Mourinho amezipuuza tetesi zinazoendelea kuenea kwamba yuko mbioni kurejea tena katika kikosi cha Real Madrid akiwa kocha mkuu.

Tetesi hizi zimekuwa zikienea kwa kasi kufuatia matokeo duni ya timu hiyo chini ya mkufunzi Zinedine Zidane, huku kichapo cha majuzi cha 3-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain (PSG) katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kikiendelea kuwauma sana wakuu wa miamba hao wa soka ya La Liga.

Zidane alirejea uwanjani Santiago Bernabeu katikati ya msimu uliopita lakini akawaongoza waajiri wake kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali lililotawaliwa na watani wao wakuu, Barcelona.

Mourinho amesema si rahisi kwa kocha Zidane kupoteza kazi yake kambini mwa Real, kwani ni mtu anayeweza kujirekebisha haraka na kukichochea upya kikosi chake kuanza tena kusajili ushindi.

“Ni ukweli mambo hayaendi vizuri pale Bernabeu, lakini si kazi yangu kuanza kuivizia ajira ya mwenzangu. Katika hii kazi yetu ya ukufunzi, heshima ni kitu muhimu sana,” alisema Mourinho mwenye umri wa miaka 56.

Tangu atimuliwe na Man-United kwa sababu ya matokeo duni mnamo Desemba 2018, Mourinho bado hajapata kazi.

Hata hivyo, amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kupokezwa mikoba ya timu mbalimbali za taifa na hata vikosi vya Real au Barcelona ambavyo kwa sasa vinasuasua ligini.

Wakati huo huo, klabu ya Wolves inakaribia kukamilisha mpango wa kumpa mkataba mpya kiungo wao matata Joao Moutinho, raia wa Ureno ambaye amekuwa tegemeo kubwa kwenye safu ya kati kambini mwa waajiri wake na timu ya taifa.

Moutinho amekuwa na ushawishi mkubwa uwanjani tangu alipotua Wolves mnamo Julai 2018 akitokea AS Monaco ya Ufaransa.

Umri

Kufikia sasa, amecheza zaidi ya mechi 50 katika mashindano tofauti. Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 33, Wolves wanapanga kumbakiza kiungo huyo ambaye mkataba wake unafika tamati mwishoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Taarifa za mtandao wa Wolves zimesema kwamba klabu hiyo ipo katika hatua nzuri za makubalianao ya kumpa Moutinho huyo mkataba mpya wa miaka miwili.

Upande wa mchezaji huyo umesema kiungo huyo yuko tayari kuendelea kuichezea Wolves kwa zaidi ya miaka miwili.