Michezo

Real kujinasia kiungo Van de Beek badala ya Pogba

August 6th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

REAL Madrid wamefichua azma ya kumsajili kiungo Donny van de Beek wa Ajax Amsterdam iwapo watashindwa kabisa kumshawishi Paul Pogba wa Manchester United kubanduka uwanjani Old Trafford.

Hatua hii ya Real ni jambo ambalo kocha Zinedine Zidane amekiri kwamba inavunja moyo na kushusha zaidi motisha iliyokuwa imeanza kumvaa Pogba, 26.

Kiini cha Real kuyahemea maarifa ya Van de Beek kinachochewa na kauli ya hivi karibuni ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye amesisitiza kuwa Pogba atazidi kuvalia jezi za Man-Utd msimu ujao kwa kuwa anayafurahia sasa maisha ugani Old Trafford.

Hatua ya Solskjaer kumuacha Pogba nje ya kikosi cha Man-Utd kilichochuana kirafiki na AC Milan jijini Cardiff wikendi jana iliwaaminisha wengi kwamba kiungo huyo wa zamani wa Juventus alikuwa pua na mdomo na kutua Real.

Mengi ya magazeti nchini Uingereza yaliripoti kwamba kusazwa kwa Pogba uwanjani Old Trafford wakati wa mchuano huo kulikuwa zao la mgomo baridi uliopania kuwashinikiza waajiri wake kumwachilia.

Mbali na tetesi kuhusu uwezekano wa kutua Real, Pogba amekuwa pia akihemewa pakubwa na Juventus na Barcelona ambao wapo radhi kuagana na kiungo matata mzawa wa Brazil, Philippe Coutinho.