Michezo

Real Madrid, Bayern na Man U sasa zamezea mate Salah

June 4th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara sita wa Klabu Bingwa Ulaya, Liverpool wana kibarua kigumu kuendelea kumkwamilia mshambuliaji Mohamed Salah baada ya ripoti kwamba Real Madrid, Manchester United na Bayern Munich wanamezea mate raia huyu wa Misri

Winga huyu mwenye mguu hatari wa kushoto alipachika penalti katika dakika ya pili baada ya Mfaransa Moussa Sissoko kuonekana kunawa krosi ya raia wa Senegal, Sadio Mane ndani ya kisanduku kabla ya Mbelgiji mwenye asili ya Kenya, Divock Origi kuzamisha chombo cha Tottenham Hotspur kabisa katika fainali ya Klabu Bingwa nchini Uhispania hapo Juni 1.

Salah ni mchezaji wa tatu Mwarabu kutwaa taji la Klabu Bingwa baada ya raia wa Algeria, Rabah Madjer kunyakua taji la mwaka 1987 akiwa FC Porto nchini Ureno na Mmoroko Achraf Hakimi mwaka 2018 akiwa Real Madrid.

Ripoti nchini Uhispania zinasema Madrid inatafuta huduma za Salah. Mabingwa hawa mara 13 wa Bara Ulaya walijaribu kumsaini kutoka Liverpool mwisho wa msimu 2017-2018 alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza, lakini Liverpool ikaitisha kitita cha kutisha cha Sh23 bilioni kilichofanya Wahispania hao kujiondoa.

Ripoti hiyo kutoka gazeti la AS inasema kwamba macho ya miamba wa Ujerumani, Bayern Munich pamoja na mibabe Manchester United yamekwamilia uwanjani Anfield kuangalia hali ilivyo baada ya wote kuwa na msimu mbaya katika Klabu Bingwa.