Michezo

Real Madrid mara hii hawaendi popote UEFA, ManCity wana nafasi kubwa

December 17th, 2018 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

KUKAMILIKA kwa kampeni za makundi katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wiki jana kulipisha droo ya hatua ya 16-bora itakayofanyika leo jijini Nyon, Uswisi.

Timu 16 zilizotinga awamu ya mwondoano zitafahamu wapinzani wazo wa hatua ijayo itakayopigwa kati ya Febaruari 12 na Machi 13, 2019.

Miongoni mwa wawakilishi wa EPL katika kipute hicho, ni Manchester City ndio waliotia fora zaidi kwa kuwapiku Lyon, Shakhtar Donetsk na Hoffenheim na kumaliza kileleni kwa Kundi F. Vikosi vingine vya EPL -Tottenham Hotspur, Liverpool na Manchester United viliambulia nafasi za pili kutoka makundi B, C na H mtawalia.

Ufanisi wa Man-City unatarajiwa kuwapa nafuu ya kukutana na mpinzani mnyonge katika hatua ya 16-bora; ima awe Atletico Madrid, Schalke, Ajax au Roma ambao waliambulia nafasi za pili katika makundi A, D, E na G mtawalia.

Tottenham ambao walimaliza nyuma ya Barcelona katika Kundi A, wanatarajiwa kukutanishwa na mpinzani mkali zaidi katika soka ya bara Ulaya. Hali sawa na hiyo inawasubiri Man-United na Liverpool ambao walizidiwa maarifa na Real Madrid katika fainali ya muhula jana.

Licha ya kusuasua sana hadi kufikia sasa katika kampeni za EPL, Man-United waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Juventus katika Kundi H kwenye UEFA.

Man-United, Ajax na Schalke ni miongoni mwa wapinzani walioambulia nafasi za pili ambao kila kikosi kilichomaliza kileleni mwa kundi kingetamani sana kukutana nao.

Kati ya klabu zilizotawala vilele vya makundi yao, ni Porto pekee ndiyo inayoonekana kuwa dhaifu katika tapo linalowajumuisha pia Barcelona, Bayern Munich, Borussia Dortmund, Juventus, Man-City, PSG na mabingwa watetezi wa UEFA, Real Madrid.

Porto kwa sasa wanatazamiwa kukutana ama na Liverpool, Tottenham au Man-United.

Tangu kocha Lucien Favre apokezwe mikoba ya Dortmund, kikosi hicho kilichowapiga kumbo Atletico, Club Brugge na Monaco katika Kundi A kinajivunia ufufuo mkubwa kiasi kwamba hakuna mpinzani yeyote ambaye angetamani kukutana nao.

Kufikia sasa, Dortmund wamepoteza mchuano mmoja pekee katika mapambano yote ya msimu huu na tayari wanaselelea kileleni mwa Bundesliga huku wakidumisha pengo kubwa la alama kati yao na Monchenggladbach ambao ni wa pili jedwalini.

Real wamenyanyua mataji manne ya UEFA katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Matatu kati ya mataji hayo yaliwajia kwa mfululizo wa miaka misimu mitatu iliyopita chini ya kocha Zinedine Zidane ambaye kwa sasa anahusishwa na Man-United na Bayern Munich.

Kwa mtazamo wangu, sioni kabisa uwezekano wa Real kuendeleza ubabe wao huo msimu huu chini ya mkufunzi mpya Santiago Solari. Kwa hakika, Real ambao pia wanasuasua katika La Liga, ni wafalme wa UEFA ambao wanachechemea tu msimu huu.

Kati ya klabu zote zinazonogesha kivumbi cha EPL, ni Man-City ambao wanatarajiwa kukutana sasa na Schalke kutoka Ujerumani, ndio wameonesha ishara na uwezo wa kuyakabili vilivyo mawimbi ya ushindani katika kipute cha UEFA msimu huu.

Si ajabu mabingwa hao watetezi wa EPL wajikakamue vilivyo katika michuano iliyopo mbele yao kiasi cha kutawazwa wafalme wa UEFA hatimaye.

Mbali na Man-City, ninahisi kwamba Barcelona na PSG pia wana fursa nzuri zaidi ya kutawazwa mabingwa wa UEFA msimu huu.