Real Madrid na AC Milan nguvu sawa huku Bale akipoteza penalti

Real Madrid na AC Milan nguvu sawa huku Bale akipoteza penalti

Na MASHIRIKA

GARETH Bale alikuwa sehemu sehemu ya kikosi kilichowajibishwa na kocha Carlo Ancelotti wa Real Madrid dhidi ya AC Milan mnamo Jumapili.

Timu hizo ziliambulia sare tasa.

Bale alirejea kambini mwa Real mwishoni mwa Julai 2021 baada ya mkataba wake wa mkopo kambini mwa Tottenham Hotspur kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Akivalia jezi nambari 50 mgongoni katika mechi ya kirafiki dhidi ya AC Milan, Bale alichezeshwa kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza. Mchuano huo uliosakatiwa nchini Austria, ulikamilika kwa sare tasa.

Bale, 32, alipoteza penalti wakati wa mechi hiyo mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Nyota huyo hakuwa amewahi kuchezea Real tangu Juni 2020 baada ya kutofautiana kimawazo na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Zinedine Zidane.

Lakini baada ya Ancelotti kuajiriwa tena na Real mwishoni mwa msimu wa 2020-21, kocha huyo raia wa Italia alifichua azma ya kumpa Bale fursa ya kufufua makali yake uwanjani Bernabeu.

Bale ambaye amesaidia Real kuzoa mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) angali na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Real watafungua rasmi kampeni zao za msimu mpya wa 2021-22 dhidi ya Alaves mnamo Agosti 14, 2021. Bale alifungia Spurs mabao 17 kutokana na mechi 34  za msimu wa 2020-21. Kati ya mechi hizo, 10 zilikuwa za EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mturuki mwandani wa Dkt Ruto afurushwa nchini

Isuzu EA yapangia Kipchoge mapokezi motomoto