Michezo

Real Madrid na Bayern Munich wanakata mzizi leo

May 8th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

REAL Madrid watakuwa nyumbani ugani Santiago Bernabeu leo usiku kukaribisha Bayern Munich katika mkondo wa pili wa nusu fainali ya Klabu Bingwa barani Ulaya (Uefa) ambapo mshindi atatinga fainali ya michuano hiyo.

Zilipokutana katika pambano la mkondo wa kwanza uwanjani Allianz Arena, timu hizi ziliagana kwa sare ya 2-2, lakini wenyeji wanatarajiwa kupata ushindi katika mechi hii ya marudiano kutokana na fomu yao nzuri.

Tayari kikosi hicho cha kocha Carlo Ancelotti kimetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), lakini kinaendelea kutesa wapinzani katika mechi zilizobaki kwenye ligi hiyo.

Matokeo hayo mazuri katika msimu huu ni pamoja na ushindi wa mwishoni mwa wiki wa 3-0 dhidi ya Cadiz katika mechi ya La Liga.

Kikosi hicho kimejiimarisha kitaaluma na hakiyumbiki kinapokuwa uwanjani hasa katika mechi muhimu.

Wakati kikiandikisha ushindi huo wa 3-0 dhidi ya Cadiz, Bayern Munich ilicharazwa 3-1 na Stuttgart, kichapo ambacho kimeshusha morali ya mashabiki wao.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Madrid ugani Allianz, Bayern walitawala kwa kiasi kikubwa, lakini hawatarajiwi kuendeleza ubabe huo ugenini.

Ufanisi mkubwa wa kiufundi wa nyota Rodrygo Silva de Geos unatarajiwa kuongezea Madrid nguvu zaidi katika juhudi zao za kutafuta ushindi leo usiku. Raia huyo wa Brazil amekuwa akitegemewa katika usambazaji wa mipira, na uwepo wake utasaidia Madrid kwa kiasi kikubwa katika mechi hii muhimu.

Kwa upande wa Bayern, Harry Kane ni miongoni mwa wachezaji watakaotegemewa, kutokana na kipaji chake cha kufunga mabao. Ujasiri wake kupiga mpira akitumia miguu yote umekuwa wa hali ya juu.

Uwezo wake wa kipekee awapo hewani umezidi washambuliaji wenzake wanaocheza kwenye ligi kubwa barani Ulaya. Kiwango chake kwa sasa ni bora, na bila shaka atakuwa tishio kwa Real Madrid.

Hata hivyo, Real Madrid hawajashindwa na Bayern katika mechi nane zilizopita. Katika mechi 16, Madrid wamekuwa wakifunga langoni pa Bayern.

Isitoshe, katika mechi tisa, Bayern haijashinda timu yoyote ya kocha Ancelotti katika michuano hii ya Klabu Bingwa.

Mshindi wa pambano hili atakutana na mshindi kati ya PSG na Borussia Dortmund waliopangiwa kukutana na jana usiku ugani Parc de Princes jijini Paris, Ufaransa.

Nusu fainali ya leo kati ya Real Madrid dhidi ya Bayern Munich itasakatiwa katika uga wa Santiago Bernabeu, saa mbili usiku.