Real Madrid na Villarreal ni nguvu sawa La Liga

Real Madrid na Villarreal ni nguvu sawa La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid na Villarreal waliendeleza rekodi nzuri za kutoshindwa katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu baada ya kuambulia sare tasa mnamo Jumamosi usiku ugani Santiago Bernabeu.

Chini ya mkufunzi Carlo Ancelotti, Real walijibwaga ugani wakijivunia kufunga mabao 21 kutokana na mechi sita za ufunguzi wa msimu huu ligini.

Kombora la Karim Benzema na mpira wa kichwa uliopigwa na Isco ndiyo yaliyokuwa majaribio ya pekee ya Real langoni pa Villarreal waliotegemea pakubwa maarifa ya Geronimo Rulli.

Ingawa Villarreal walipata nafasi chache za kufunga bao, walipoteza fursa nzuri zaidi ya kupata bao la pekee na la ushindi kupitia Arnaut Danjuma aliyemwajibisha vilivyo kipa Thibaut Courtois.

Licha ya sare hiyo, Real wangali kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 17, tatu zaidi kuliko Sevilla na mabingwa watetezi Atletico. Ni pengo la alama tatu ndilo linatamalaki kati ya Real na Sevilla waliokung’uta Espanyol 2-0 katika gozi jingine la Jumamosi.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Real kusajili sare katika La Liga chini ya kocha Ancelotti ambaye sasa amesimamia mechi 83 za kikosi hicho katika awamu mbili za ukufunzi.

Villarreal ya kocha Unai Emery sasa inashikilia nafasi ya 10 kwa alama nane sawa na Mallorca na Osasuna licha ya kutoshindwa. Kikosi hicho kimeambulia sare tano kati ya michuano sita iliyopita ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nyuki wavamia na kumuua mzee aliyehudhuria mazishi ya mjukuu

JAMVI: Nyota ya kisiasa ya Karua inaingia doa?