Michezo

Real Madrid waalika PSG kwa mtihani mkali wa Uefa

November 26th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

REAL Madrid watapania leo Jumanne kulipiza kisasi dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha uwanjani Santiago Bernabeu, Uhispania.

Katika mechi nyingine inayotarajiwa kuwa ya kusisimua zaidi, Juventus ambao ni miamba wa soka ya Italia, watakuwa wenyeji wa Atletico Madrid kutoka Uhispania.

Manchester City na Tottenham Hotspur ambao ni miongoni mwa wawakilishi wa Uingereza katika kivumbi cha UEFA msimu huu, watawakaribisha Shakhtar Donetsk na Olympiacos mtawalia.

Kichapo cha 3-0 ambacho Real walipokezwa na PSG katika mchuano wa mkondo wa kwanza uwanjani Parc des Princes mnamo Septemba 2019, kilimsaza kocha Zinedine Zidane katika presha kubwa.

Kikubwa zaidi kilichomning’iniza padogo kocha Zidane mwishoni mwa mchuano huo, ni kwamba PSG walisajili ushindi huo mnono bila ya kujivunia huduma za wavamizi nyota Neymar Jr, Edinson Cavani na Kylian Mbappe.

Mabao mawili ya PSG wakati wa mchuano huo yalijazwa kimiani na Angel Di Maria ambaye alikizamisha kabisa chombo cha Real ambao ni waajiri wake wa zamani.

Kinachostahili kuwa kiini cha hofu zaidi kambini mwa Real ni kwamba masogora hao watatu wa PSG wamerejea na ujio wao utatazamiwa kuwa kiini cha hamasa ya miamba hao wa Ufaransa ambao wamekuwa wakimtegemea sana Mauro Icardi katika safu ya mbele.

Hata hivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Zidane amerejesha hali ya uthabiti kambini mwa Real ambao wanapigiwa upatu wa kusonga mbele kwa pamoja na PSG kutoka Kundi A.

Nyota Eden Hazard anatazamiwa kutamba zaidi dhidi ya PSG ambao waliwahi kumnyemelea pakubwa katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita alipokuwa akivalia jezi za Chelsea.

Kukosekana kwa James Rodriguez, Nacho, Marco Asensio na Lucas Vazquez kutakuwa kiini cha kuwajibishwa zaidi kwa Hazard anayepigiwa kushirikiana na Gareth Bale na Karim Benzema katika safu ya mbele ya Real.

PSG waliwakaribisha Neymar na Mbappe kikosini mwao mnamo Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) iliyowakutanisha na Lille. Wawili hao wanapigiwa upatu wa kuunga kikosi cha kwanza dhidi ya Real.

RATIBA Leo Jumanne:

Lokomotiv na Leverkusen, Real Madrid na PSG, Man-City na Shakhtar, Galatasaray na Club Brugge, Tottenham na Olympiacos, Juventus na Atletico, Red Star Belgrade na Bayern, Atalanta na Dinamo Zagreb;

Jumatano:

Zenit na Lyon, Barcelona na Dortmund, Lille na Ajax, Liverpool na Napoli, Valencia na Chelsea, Slavia Praha na Inter, Genk na Salzburg, Leipzig na Benfica.