Michezo

Real Madrid wacharaza Eibar na kufikia Atletico Madrid kileleni mwa jedwali la La Liga

December 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipepeta Eibar 3-1 na kuendeleza presha kwa viongozi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid.

Mechi hiyo ilikuwa ya nne mfululizo kwa Real kusajili katika kampeni za La Liga msimu huu.

Karim Benzema alifungulia Real ukurasa wa mabao katika dakika ya sita kabla ya kuchangia mawili mengine yaliyofumwa wavuni na Luka Modric na Lucas Vazquez katika dakika za 13 na 90 mtawalia.

Bao la Eibar lilifumwa wavuni kupitia Kike Garcia katika dakika ya 28.

Ushindi kwa Real ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Zinedine Zidane uliwapaisha hadi nafasi ya pili jedwalini kwa alama 29 sawa na Atletico ya kocha Diego Simeone.

Real Sociedad wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 26, moja nyuma ya nambari nne Villarreal.

Atletico watakuwa wageni wa Sociedad mnamo Disemba 22 huku Real almaarufu Los Blancos wakivaana na Granada.