Real Madrid wacharaza Sociedad na kufungua pengo la alama nane kileleni mwa jedwali la La Liga

Real Madrid wacharaza Sociedad na kufungua pengo la alama nane kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walifungua mwanya wa alama nane kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kuwatandika Real Sociedad 2-0 mnamo Jumamosi.

Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Real wamejizolea alama 39 kutokana na mechi 16 zilizopita na ni mgongo wao unasomwa kwa karibu na Sevilla kwa pointi 31.

Vinicius Jr alifungulia Real ukurasa wa mabao katika dakika ya 47 kabla ya Luka Jovic kupachika wavuni goli la pili dakika 10 baadaye.

Bao la Jovic aliyejaza nafasi ya fowadi Karim Benzema katika kipindi cha kwanza, lilikuwa lake la kwanza msimu huu ndani ya jezi za Real.

Real kwa sasa watajiandaa kwa gozi kali dhidi ya Atletico Madrid mnamo Disemba 12 wakiwa na motisha tele ikizingatiwa kwamba Atletico ya kocha Diego Simeone ilipepetwa 2-1 na Mallorca katika uwanja wao wa nyumbani wa Wanda Metropolitano.

Atletico ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga, waliteremka hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 29.

Ilikuwa mechi ya pili mfululizo kwa Real Sociedad kupoteza baada ya kujivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi 13 za La Liga. Kikosi hicho kwa sasa kinakamata nafasi ya tano jedwalini kwa alama 29.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kanisa laomba usalama uimarishwe msimu wa sherehe

Origi abeba Liverpool dhidi ya Wolves ligini

T L