Michezo

Real Madrid wacharaza Valladolid na kupaa hadi kileleni mwa jedwali la La Liga

October 2nd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Vinicius Junior alitokea benchi na kufungia Real Madrid bao la pekee na la ushindi dhidi ya Real Valladolid katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyosakatiwa uwanjani Santiago Bernabeu mnamo Septemba 30, 2020.

Mchuano huo ulikuwa wa tatu kwa Real kutandaza ligini hadi kufikia sasa msimu huu wa 2020-21.

Katika mechi mbili za kwanza zilizosakatwa na Real ugenini, masogora hao wa kocha Zinedine Zidane waliridhika na alama nne pekee baada ya kulazimishiwa sare tasa na Real Sociedad mnamo Septemba 20, 2020 kisha kutoka nyuma na kuwalaza Real Betis 3-2 mnamo Septemba 26.

Kipa Roberto Jimenez alifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito ya Federico Valverde na Luka Jovic katika dakika za mwisho wa kipindi cha pili.

Ingawa hivyo, alikuwa ni Vinicius Jr aliyeleta kasi na nguvu mpya kwenye safu ya ushambulizi ndiye aliyewapa Real alama zote tatu katika mchuano huo kupitia goli lake la dakika ya 65.

Ushindi kwa Real uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama saba sawa na Getafe, Villarreal na Valencia.

MATOKEO YA LA LIGA (Septemba 30, 2020):

Huesca 0-0 Atletico Madrid

Villarreal 3-1 Alaves

Eibar 0-1 Elche

Real Madrid 1-0 Valladolid

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO