Na MASHIRIKA
REAL Madrid walipoteza fursa ya kupunguza pengo la alama kati yao na Barcelona kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya Real Sociedad kuwalazimishia sare tasa ugani Bernabeu.
Matokeo hayo yaliacha mabingwa hao watetezi wa La Liga katika nafasi ya pili kwa pointi 42, tano nyuma ya viongozi Barcelona ambao pia wametandaza mechi 18.
Sociedad wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 39, tano zaidi kuliko Atletico Madrid wanaofunga mduara wa nne-bora baada ya kupepeta Osasuna 1-0 uwanjani El Sadar. Bao la pekee la Atletico ambao wamesakata michuano 19 sawa na Sociedad, lilipachikwa wavuni na Saul Niguez.
Real Valladolid nao walijiondoa katika orodha ya vikosi vitatu vya mwisho jedwalini baada ya kukomoa Valencia 1-0. Sasa wana alama 20 baada ya mechi 19, sawa na Valencia, Espanyol na Celta Vigo waliotandika Athletic Club Bilbao 1-0.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO