Real Madrid wakamilisha kampeni za msimu huu wa 2020-21 mikono mitupu

Real Madrid wakamilisha kampeni za msimu huu wa 2020-21 mikono mitupu

Na MASHIRIKA

LICHA ya kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Villarreal katika mchuano wa mwisho wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Mei 22, 2021, Real Madrid walikosa kuhifadhi taji la kipute hicho.

Hii ni baada ya Atletico Madrid nao kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Real Valladolid katika mechi yao ya mwisho msimu huu wa 2020-21 na kujitwalia ubingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza tangu 2013-14.

Chini ya kocha Diego Simeone ambaye ni raia wa Argentina, Atletico walikamilisha muhula kwa alama 86, mbili zaidi kuliko nambari mbili Real na saba mbele ya Barcelona walioambulia nafasi ya tatu.

Ili kuhifadhi ubingwa wa La Liga, Real walihitajika kushinda Villarreal nao Atletico waliokuwa wakiwania taji lao la 11 ligini wapoteze dhidi ya Valladolid. Real ya kocha Zinedine Zidane sasa imekamilisha kampeni za msimu huu bila ya kujizolea taji lolote.

Miamba hao walibanduliwa mapema kwenye soka ya Copa del Rey kabla ya Chelsea kuwadengua kwenye nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa jumla ya mabao 3-1.

Wakicheza dhidi ya Real, Villarreal waliwekwa kifua mbele na fowadi Yeremi Pino katika dakika ya 20 kabla ya Karim Benzema kusawazisha mambo kunako dakika ya 87. Kiungo Luka Modric ndiye alizamisha kabisa chombo cha Villarreal sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Chini ya mkufunzi Unai Emery aliyewahi kudhibiti mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG) na Arsenal, Villarreal kwa sasa wanajiandaa kwa fainali ya Europa League dhidi ya Manchester United mnamo Mei 26 jijini Gdansk, Poland.

MATOKEO YA LA LIGA (Mei 22, 2021):

Celta Vigo 2-1 Real Betis

Eibar 0-1 Barcelona

Elche 2-0 Bilbao

Huesca 0-0 Valencia

Osasuna 0-1 Sociedad

Real Madrid 2-1 Villarreal

Valladolid 1-2 Atletico

You can share this post!

Orengo awalaumu vigogo ODM kwa kumtoroka Raila

JAMVI: Mwamko mpya Pwani 2022