Real Madrid waponda Mallorca na kurejea kileleni mwa jedwali la La Liga

Real Madrid waponda Mallorca na kurejea kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

MARCO Asensio alifunga mabao matatu na kusaidia Real Madrid kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kupepeta Mallorca 6-1 mnamo Jumatano usiku ugani Santiago Bernabeu.

Asensio alipachika wavuni mabao mawili chini ya dakika tano za kipindi cha kwanza huku Mallorca wakifungiwa na Lee Kang-in. Asensio ambaye ni raia wa Uhispania, aliagana na Mallorca mnamo 2015 na kuyoyomea Real. Alifanya mambo dhidi ya Mallorca kuwa 4-1 dakika 10 baada ya mwanzo wa kipindi cha pili.

Karim Benzema aliwafungulia Real ukurasa wa mabao katika dakika ya tatu kabla ya kupachika wavuni goli la tano la waajiri wake katika dakika ya 78.

Isco ndiye alizamisha kabisa chombo cha Mallorca kwa kufuma wavuni bao la sita la Real kunako dakika ya 84.

Awali, Atletico Madrid walikuwa wametua kileleni mwa jedwali la La Liga baada ya kucharaza Getafe 2-1 mnamo Jumanne. Mabingwa hao watetezi wa La Liga sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 14, mbili nyuma ya viongozi Real wanaotiwa makali na kocha Carlo Ancelotti. Atletico na Real hawajapoteza mechi yoyote kati ya sita zilizopita.

Benzema kwa sasa anajivunia mabao manane na kuchangia mengine saba kutokana na mechi sita zilizopita ambazo amechezea Real muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Fred Mutwiri

West Ham wadengua Man-United kwenye raundi ya tatu ya...