Michezo

Real Madrid warejea kileleni mwa La Liga katika gozi lililoshuhudia Mallorca wakiwajibisha kinda

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Vinicius Junior na beki Sergio Ramos walicheka na nyavu za Mallorca na kuchochea Real Madrid kusajili ushindi wa 2-0 uliowarejesha kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Masogora hao wa kocha Zinedine Zidane sasa wanajivunia alama 68 sawa na Barcelona japo Real wanaorodheshwa juu ya mabingwao hao watetezi kutokana na ubora wa rekodi yao.

Vinicius ambaye ni mzawa wa Brazil alitikisa nyavu za Mallorca kunako dakika ya 19 kabla ya Ramos kufunga la pili katika dakika ya 56 kupitia mpira wa ikabu.

Mallorca walimpa chipukizi Luka Romero, 15, nafasi katika kipindi cha pili na kumfanya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuchezeshwa katika historia ya La Liga.

Mechi hiyo ilikuwa pia fursa ya kwanza kwa fowadi Gareth Bale kuwahi kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Real tangu Februari 2020.

Hata hivyo, mchango wa sogora huyo mzawa wa Wales haukuhisika sana uwanjani huku jaribio lake langoni pa Mallorca likidhibitiwa vilivyo na kipa Manolo Reina aliyetatizwa sana baadaye na Eden Hazard na Karim Benzema.

Real wanasalia sasa na mechi saba zaidi na ushindi katika michuano hiyo yote utawazolea ubingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza tangu 2017. Kwa upande wao, Mallorca wanasalia kuning’inia padogo mkiani kwa alama 26, mbili pekee kuliko Espanyol wanaokokota nanga.