Real Madrid watandika Celta Vigo ugani Bernabeu na kurejea kileleni mwa jedwali la La Liga

Real Madrid watandika Celta Vigo ugani Bernabeu na kurejea kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walirejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumamosi usiku baada ya kuwatandika Celta Vigo 2-0 katika mechi iliyochezewa uwanjani Santiago Bernabeu.

Celta Vigo walijibwaga ugani kwa minajili ya pambano hilo wakijivunia rekodi ya kutoshindwa ligini tangu Novemba 21. Hata hivyo, walijipata nyuma baada ya dakika sita pekee za kipindi cha kwanza kutokana na bao la Lucas Vazquez aliyejaza kimiani mpira aliopokezwa na Marco Asensio.

Bao la pili la Real lilifumwa wavuni na Asensio katika dakika ya 53 baada ya kuandaliwa krosi safi na Casemiro.

Makali ya Celta Vigo yalididimia kabisa katika kipindi cha pili baada ya fowadi wao tegemeo Iago Aspas kupata jeraha lililomweka katika ulazima wa kuondoka uwanjani.

Jaribio la pekee la Celta Vigo langoni mwa wenyeji wao ni kombora lililovurumishwa na kiungo Santi Mina katika goli la kipa Thibaut Courtois kunako dakika ya 67.

Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 36, moja kuliko nambari mbili Atletico Madrid ambao wana mechi tatu zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo tayari imepigwa na Real ya kocha Zinedine Zidane. Chini ya mkufunzi Diego Simeone, Atletico wamepangiwa kuvaana na Alaves ugenini mnamo Januari 3, 2021.

MATOKEO YA LA LIGA (Januari 2, 2021):

Real Madrid 2-0 Celta Vigo

Villarreal 2-1 Levante

Real Betis 1-1 Sevilla

Getafe 0-1 Real Valladolid

You can share this post!

CHOCHEO: Kupata mchumba si muujiza, lazima utoke ukutane na...

Arsenal watangaza rasmi ufufuo wao ligini kwa kupokeza West...