Real Madrid wazima ndoto ya Liverpool katika UEFA kwa mara ya tatu mfululizo

Real Madrid wazima ndoto ya Liverpool katika UEFA kwa mara ya tatu mfululizo

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Liverpool kupiga hatua zaidi kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu yalizimwa na mabingwa watetezi Real Madrid mnamo Jumatano usiku kwa kichapo cha 1-0 ugani Bernabeu na hivyo kubanduliwa kwenye hatua ya 16-bora kwa jumla ya mabao 6-2.

Ilikuwa mara ya tatu mfululizo kwa Real kushinda Liverpool katika hatua mbalimbali za kipute cha UEFA.

Liverpool walishuka dimbani wakitegemea huduma za washambuliaji wanne huku wakilenga kuendeleza historia ya kuwahi kutoka chini kwa mabao 3-0 na kudhalilisha Barcelona kwa mabao 4-0 katika mkondo wa pili wa nusu-fainali ya UEFA mnamo 2018-19.

Real, wanaowinda taji la 15 la UEFA, walifunga bao lao la pekee na la ushindi katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora dhidi ya Liverpool mnamo Jumatano kupitia kwa fowadi mzoefu Karim Benzema katika dakika ya 78. Goli hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Vinicius Jr.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool wangepoteza mechi hiyo kwa zaidi ya bao moja iwapo kipa Alisson Becker angekosa kujituma maradufu na kudhibiti vilivyo makombora mazito aliyoelekezewa na Vinicius pamoja na Eduardo Camavinga.

Hata hivyo, huenda mambo yangalikuwa tofauto iwapo fowadi wa Liverpool, Darwin Nunez, angalitumia vyema nafasi ya wazi aliyopata katika dakika ya sita.

Kichapo cha jumla ya mabao 6-2 kutoka kwa Real ndicho kinono zaidi kwa Liverpool kuwahi kupokezwa katika historia ya UEFA.

Liverpool walipigwa na Real 1-0 kwenye fainali ya UEFA 2021-22 jijini Paris, Ufaransa na sasa wana kibarua kigumu cha kufuzu kwa kipute hicho msimu ujao wa 2023-24. Baada ya mechi 26, kikosi hicho kinakamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 42, sita zaidi nyuma ya nambari nne Tottenham Hotspur ambao wamesakata mechi moja zaidi.

Pigo la pekee kwa Real ni jeraha lililomlazimisha kocha Carlo Ancelotti kuondoa Benzema uwanjani katika kipindi cha pili baada ya kufunga bao. Hata hivyo, nyota huyo raia wa Ufaransa amesisitiza kwamba yuko katika hali shwari ya kuunga kikosi kitakachotegemewa na waajiri wake Real dhidi ya Barcelona kwenye El Clasico mnamo Machi 19, 2023.

Ilikuwa mara ya 92 kwa kikosi kimoja kupoteza mechi ya mkondo wa kwanza ya UEFA kwa mabao matatu au zaidi. Vikosi vyote 92 vilivyowahi kupokezwa kichapo sawa na hicho vilibanduliwa.

Mnamo 2005, Liverpool walitoka chini kwa mabao 3-0 na kupepeta AC Milan ya kocha Ancelotti kwa penalti 3-2 baada ya kuambulia sare ya 3-3 katika muda wa ziada. Miaka mitatu iliyopita, walipoteza 3-0 dhidi ya Barcelona ugenini kabla ya kubatilisha ushindi huo kwa wa 4-0 nyumbani na kutinga fainali.

Liverpool waliwajibishwa mafowadi wanne – Diogo Jota, Nunez, Mohamed Salah na Cody Gakpo dhidi ya Real katika mkondo wa pili ugani Bernabeu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wanaompangia Raila maovu wajue Mwenyezi Mungu atamlinda...

Rais Ruto ateua CAS 50 kusimamia wizara 22

T L