Real Madrid yavuna ushindi mwembamba dhidi ya Atalanta kwenye UEFA ugenini

Real Madrid yavuna ushindi mwembamba dhidi ya Atalanta kwenye UEFA ugenini

Na MASHIRIKA

FERLAND Mendy alifunga bao la dakika za mwisho na kusaidia Real Madrid kusajili ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Atalanta ya Italia katika mkondo wa kwanza wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 24, 2021.

Atalanta walikamilisha mchuano huo uliochezewa katika uwanja wao wa nyumbani wa Di Bergamo nchini Italia wakiwa na wachezaji 10 ugani baada ya kiungo Remo Freuler ambaye ni raia wa Uswisi kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 17. Freuler alipokezwa adhabu hiyo kali kwa kumzuia Mendy kufunga bao la wazi.

Atalanta waliozidiwa maarifa katika kila idara walielekeza kombora moja pekee langoni mwa Real ambao watakuwa wenyeji wa mkondo wa pili mnamo Machi 16, 2021.

Real walikosa huduma za idadi kubwa ya wanasoka wao wa kikosi cha kwanza wakiwemo Karim Benzema, Eden Hazard, Dani Carvajal na nahodha Sergio Ramos.

Mbali na Mendy, wanasoka wengine walioridhisha zaidi kambini mwa Real dhidi ya Atalanta ni Isco na Marco Asensio waliomtatiza pakubwa kipa Pierluigi Gollini katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Kuchapwa kwa Atalanta kuliendeleza rekodi yao duni ya kutoshinda mechi yoyote ya nyumbani kwenye kampeni za UEFA msimu huu.

Wakati wa marudiano, Real ya kocha Zinedine Zidane itakuwa ikiwania kufuzu kwa hatua nyingine ya mwondoano ya UEFA kwa mara ya 13 kutokana na misimu 14 iliyopita. Hii ni baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kusonga mbele kwenye UEFA baada ya hatua ya makundi katika kipindi cha misimu 24 mfululizo.

Real na Bayern Munich ya Ujerumani sasa wameshinda jumla ya washindani 60 tofauti kwenye soka ya UEFA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KAMAU: Teknolojia: Afrika isisingizie wakoloni kuachwa nyuma

Pep ataka Manchester City wawe katili zaidi licha ya...