Michezo

Real Sociedad yaondoka kileleni mwa jedwali la La Liga baada ya kutandikwa na Barcelona

December 17th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA walitoka nyuma na kuwacharaza Real Sociedad 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumatano.

Matokeo yalitosha kuwadondosha Sociedad kileleni mwa jedwali ambalo kwa sasa linadhibitiwa na Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone.

Kwa upande wao, Barcelona walitoka katika nafasi ya nane na kuruka hadi nafasi ya tano kwa alama 20, sita nyuma ya nambari tatu Real Madrid.

Willian Jose aliwaweka Sociedad kifua mbele katika dakika ya 27 kabla ya Jordi Alba na Frenkie de Jong kucheka na nyavu na kuvunia Barcelona alama tatu muhimu.

Antoine Griezmann alipoteza nafasi tatu za wazi za kufungia Barcelona mabao zaidi.

Real Sociedad waliojibwaga ugani wakiwa wamesajili sare katika mechi sita za awali, walidhibiti vilivyo na Barcelona licha ya mafowadi Purtu Jose na Alexander Isak kumtatiza pakubwa kipa Marc-Andre ter Stegen.

Atletico Madrid, Real Sociedad na Real Madrid wanajivunia alama 26 kila mmoja kileleni mwa jedwali la La Liga.