Michezo

Real wazamisha Eibar katika mechi ya 200 ya Zidane

June 15th, 2020 2 min read

  Na CHRIS ADUNGO

REAL Madrid walirejelea kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Eibar katika uwanja wao wa mazoezi wa Alfredo di Stefano ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 6,000 pekee.

Mchuano huo ulikuwa wa 200 kwa kocha Zinedine Zidane kusimamia kambini mwa Real ambao kwa sasa wanaukarabati uwanja wao rasmi wa nyumbani, Sanriago Bernabeu.

Kiungo Toni Kroos aliwafungulia Real ukurasa wa mabao kunako dakika ya nne kabla ya nahodha Sergio Ramos na beki Marcelo kuwafungia mengine mawili katika dakika za 30 na 37 mtawalia.

Hata hivyo, Real walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kipindi kizima cha pili huku Marcelo akionekana kumsihi kocha kumuondoa uwanjani baada ya kuzidiwa ujanja mara kadhaa na wafumaji wa Eibar.

Presha ya Eibar langoni pa Real hatimaye iliwazalishia bao lililofumwa wavuni na Pedro Bigas kunako dakika ya 60.

Zidane ambaye huu ni muhula wake wa pili wa ukufunzi kambini mwa Real, ndiye kocha wa tatu kuwahi kusimamia zaidi ya michuano 200 katika historia ya miamba hao wa soka ya Uhispania. Hadi kufikia sasa, mkufunzi huyo mzawa wa Ufaransa anajivunia kuwanyanyulia Real jumla ya mataji 10 ya haiba.

Ingawa Gareth Bale aliwajibishwa na Zidane katika kipindi cha pili, ushawishi wa nyota huyo mzawa wa Wales haukuhisika sana uwanjani.

Ushindi wa Real uliendeleza presha kwa viongozi wa jedwali Barcelona ambao waliwapepeta Mallorca 4-0 mnamo Juni 13 katika mechi iliyomshuhudia nahodha na mshambuliaji Lionel Messi akifikisha jumla ya mabao 20 katika kipute cha La Liga msimu huu.

Real ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Valencia mnamo Juni 17, wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 59, mbili nyuma ya Barcelona watakaokwaruzana leo na Leganes uwanjani Nou Camp.

Atletico Madrid waliolazimishiwa sare ya 1-1 na Athletic Bilbao uwanjani San Mames, wanakamata nafasi ya sita jedwalini kwa alama 46 sawa na Getafe waliochabangwa 2-1 na Granada. Sevilla wanashikilia nambari tatu kwa alama 50, tatu zaidi kuliko Real Sociedad wanaofunga mduara wa nne-bora. Eibar wananing’inia padogo mkiani kwa alama 27, nne mbele ya Espanyol wanaokokota nanga.