Michezo

Real yaanzisha mazungumzo kutwaa huduma za Hazard

May 13th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MABINGWA wa zamani wa La Liga Real Madrid wameanzisha mazungumzo na Chelsea ili kutwaa huduma za winga Eden Hazard kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa 2019/20.

Habari kwamba Hazard huenda akaguria Santiago Bernabeu zimekuwa zikienea na sasa inadaiwa alichezea Chelsea mechi ya mwisho kwenye sare ya 0-0 dhidi ya Leicester City Jumapili Mei 12.

Hazard amekuwa mwokozi wa Chelsea msimu huu akifunga mabao 19 na kuzalisha mengine 16 huku jitihada hizo zikifikisha Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Uropa na pia kuwawezesha kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza(EPL).

“Ndiyo nataka kuhama lakini hilo halijatimia. Bado nasubiri kujua mwelekeo wa mambo. Nimetoa uamuzi wangu ila suala hili linahusisha klabu na nitafuatilia mkondo wa mambo baada ya kucheza fainali ya ligi ya Uropa dhidi ya Arsenal,” akasema Hazard.

Hata hivyo, nyota huyo anayesakatia timu ya taifa ya Ubelgiji alisema kwamba hatili manani mazungumzo yanayoendelea kuhusu uhamisho wake akisema haja yake kuu sasa ni kushinda ligi ya Uropa.

Hata hivyo, imeripotiwa klabu zote zinaendelea na mazungumzo yatakayofanikisha uhamisho huo huku ripoti zikiashiria kwamba Hazard ameanza kuelekeza macho yake kwenye La liga msimu ujao wa 2019/20.