Michezo

Red Carpet ilivyojifua kutwaa ubingwa wa Tim Wanyonyi Super Cup

December 27th, 2018 3 min read

Na PATRICK KILAVUKA

Red Carpet ilitawazwa timu bingwa ya makala ya tano ya Tim Wanyonyi Super Cup baada ya kuilima Leeds United kwa matuta 4-2. Hii ilikuwa baada ya mchuano kuisha sare ya 1-1.

Timu hii imekuwa ikinyemelea taji hilo kwa miaka hiyo yote na kuweka matumaini yao kuwa hai wakiamini kwamba, baada ya dhidi ni faraja. Kiu ya kutwaa taji hilo kilikuwa kimewasakama kuanzia mechi ya kwanza. Walionekana kuwa na furaha mpwitompwito baada ya kulinyanyua kombe.

Kikosi cha Red Carpet kikisherekea ushindi wake dhidi ya United kipute cha Timu Wanyonyi Super Cup uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kabete. Picha/Patrick Kilavuka

“Tulifurahia sana kuibuka washindi japo wapinzani wetu nao pia alikuwa wamejiandaa na mambo uwanjani yalikuwa vita nivute hadi mwisho wakipenga,” walisema wachezaji wakipigwa picha na kombe ambalo walishinda.

Kocha wake mkuu Meshack Onchongo alisema kwamba, ingawa alikuwa ameghasika tokea kuanzishwa kwa mchuano huo, ana furaha timu imefanya vyema chini ya wadau aliowacha nyuma kuishughulikia hadi wakati fainali ambapo waliweka kombe mkononi. “Ninafuraha isiyo kifani kulibeba kombe hili ambalo limetukwepa tangu makala haya kuanzishwa na sasa sisi ni mabingwa,” asema mkufunzi huyo mkuu wa timu.

Kikosi cha Red Carpet kiamukuana na kinara wa upinzani Raila Odinga wakati mechi ya fainali ya Tim Wanyonyi Super Cup uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kabete. Picha/ Patrick Kilavuka

Safari yao katika kusaka hilo taji ilielekea kuwa nyoofu baada ya kujitosa kati mkondo wa robo fainali ambapo waliigaragaza RYSA 3-0 kupitia magoli ya Patrick Otiende dakika ya 1, Nathan Ruta akatikisa la pili dakika ya 19 na Frank Mmani akakiyumbisha chombo cha wapinzani zaidi kunako dakika ya 33.

Hatimaye, kucheza nusu fainali dhidi ya Leverkusen na kuwapachika magoli 4-2. Mabao yao yalifungwa na Edwin Amanya, Frank Mmani, Kevin Kamasi na Dennis Nyagaka ilhali Alex Maina na mchana nyavu matata Cyrus Malei walijibu mawili ya wapinzani.

Kikosi cha Red Carpet kiamukuana na kinara wa upinzani Raila Odinga wakati mechi ya fainali ya Tim Wanyonyi Super Cup uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kabete. Picha/ Patrick Kilavuka

Wapinzani wao katika fainali ( Leeds United) nao walikuwa wamefika hatua hiyo baada ya kuwasaza mahasimu wao Kangemi Wazoefu 3-2.

Carpet walikabidhiwa taji na mwandalizi wa patashika hilo Bw Tim Wanyonyi ambaye ni Mbunge wa eneo la Westlands.

Kikosi cha Red Carpet kikipasha misuli moto kabla ya mechi ya fainali ya Tim Wanyonyi Super Cup uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kabete. Picha/Patrick Kilavuka

Kikosi ambacho kilinyanyua taji hili kilikuwa kapteni Geofrey Alma, John Kamau, Kevin Isiaho, Cetrick Shimoli, Patrick Otiende, Mike Kavunga, Vitalis owiti, Nathan Luta, Godfrey Odongi, Kevin Kamasi, Maxwell Thumbs, Daniel Arasa, Stephen Herera, Frank Mmani na Dennis Getanda.

Timu sitini na moja za wanaume na kumi na mbili za wanawake kutoka wadi tano za Westlands – (Kangemi, Karura, Mt View, Parklands/Highridge, Kitisuru na Karura) zilishiriki katika kipute hicho ambacho kilizinduliwa na mdhamini wake Mbunge wa eneo hilo Tim Wanyonyi.

Kikosi cha Red Carpet. Picha/Patrick Kilavuka

“Ningependa kusema kwamba timu ambazo zitashiriki katika kinyang’anyiro hiki yapasa ziwe na ari ya kuonyesha soka tamanifu na wanasoka kudhihirisha wazi wa weledi wa talanta zao,” alisema Bw Wanyonyi ambaye aliagiza waandalizi na wadau wafanye kazi kwa njia mufti kuhakikisha dimba litafaulu kuwapa vijana fursa ya kutalii uwezo wa vipaji vyao vya kabumbu.

Katika fainali hiyo, wageni maarufu walikuwa kinara wa upinzani Bw Raila Odinga, Mbunge wa Embakasi Babu Owino, Bw George Aladwa miongoni mwa wengine.

Taji la Wanyonyi Super Cup. Picha/ Patrick Kilavuka

Kiongozi wa upinzani aliwataka wachezaji kucheza mchezo wa kuvutia na kuwa na nia ya kufikia kiwango cha wachezaji mashuhuri wa humu nchini na ughaibuni pamoja na kudumisha nidhamu ya hali ya juu.

Katika kilele cha mashindano hayo majuzi, timu bora, marafa, wachezaji na wakufunzi walituzu.

Kikosi cha Leeds United kilichoibuka cha pili bora Tim Wanyonyi Super Cup kikiwa na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga. Picha/Patrick Kilavuka

Hivyo basi upande wa madume Red Carpet walitawazwa wafalme, Leeds United wakachukua nafasi ya pili, Leverkusen nafasi ya tatu nayo Kangemi Wazoefu wakafunga mduara wa nne bora.

Upande wa akina dada, Kabete Chics walitawazwa malkia wa soka eneo la Westlands katika kipute hicho baada ya kuwashinda Patriots Queens. 2-0 kupitia mabao ambayo yalisukumwa kimiani Ann koki na Lati Atieno.

Kikosi cha Leeds United.Picha/Patrick Kilavuka

Waliobahatika mithili ya mtende kuchukua nafasi ya tatu walikuwa Kibagare Girls na Wysa Ladies wakafunga nne bora.

Mfungaji bora, upande wa vigoli alikuwa Sylvia Akoth wa Patriots Queens na Brian OKalo wa Wazoefu akaibuka upande wa wanaume.

Kipa mahiri upande wa mabinti alikuwa Judith Osimba wa Patriots wa na Mike Kavaga- wanaume.

Kikosi cha Patriots Queens ambacho kilibuka pili bora Tim Wanyonyi Super Cup.Picha/Patrick Kilavuka

Wasakataji wa soka tamanifu zaidi (MVP) walikuwa Jumila Alila ya timu ya Victoria Queens, upande wa vipusa na Cyrus Malei wa kutoka timu ya Leverkusen upande wa madume.

Refa bora upande wa wanaume alikuwa Alex Aluvaya na upande wa wanawake alikuwa Miriam Akinyi.

Kikosi cha Kabete Chics ambacho kilibuka bora Tim Wanyonyi Super Cup. Picha/Patrick Kilavuka

Kocha mahiri alikuwa Andrew Bokeya wa timu ya Chics na Daniel Liyai wa timu ya Zion.

Mabingwa wengine upande wanaume ambao wamewahi nyanyua kombe hilo ni Kangemi All Stars (2013), Amigos (2014), Kangemi Atletico (2015) na Kangemi All Stars (2016).