HabariKimataifa

Redio 24 Uganda zafungwa kwa kupeperusha matangazo ya uchawi

March 28th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

TUME  ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), imeagiza vituo 24 vya redio vifungwe mara moja kwa kupeperusha matangazo yanayohusiana na uchawi.

Shirika hilo limesema vituo hivyo vilikiuka masharti ya leseni zao licha ya kuonywa mara kadhaa. Uamuzi huo umezua hofu katika sekta ya utangazaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Msemaji wa UCC, Pamela Ankunda, aliambia gazeti la  The EastAfrican  kwamba vituo hivyo vilikuwa vimeonywa kusitisha matangazo ya kishirikina.

Tume ilitaja ilani iliyotoa Machi 24 2014 kwa vituo vyote vya redio vikome kupeperusha matangazo ya uchawi.

“Tume imefahamu kwamba licha ya  onyo la mara kwa mara, umma umelalamika dhidi ya matumizi mabaya ya mawimbi ya utangazaji, kituo chako kimeendelea kupeperusha matangazo kinyume cha sehemu ya 2 ya sheria ya uchawi,” inasem barua ya tume.

Tume hiyo pia inalaumu vituo hivyo kwa kusaidia utapeli kwa kuruhusu walaghai kutumia vituo vyao kudanganya watu kupitia matangazo  yao wakidai wana nguvu za kuponya.

Bi  Ankunda alisema vituo hivyo vitaruhusiwa kurejea hewani vikitimiza masharti ya utangazaji.

Uganda ina vituo 270 vya redio vinavyotangaza kwa mawimbi ya FM na kuna ushindani mkubwa  huku vikikubali matangazo kwa mteja yeyote aliye na pesa.

Baadhi ya wanaolipa matangazo  ya kibiashara ni madaktari wa kienyeji na waganga ambao tume inasema wanavumisha uchawi na utapeli.