Michezo

Reds wategea Leicester

October 5th, 2019 3 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

VIONGOZI wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Liverpool watawaalika leo mabingwa wa zamani Leicester City uwanjani Anfield katika mchuano utakaomkutanisha kocha Brendan Rodgers wa Leicester na waajiri wake wa zamani Liverpool.

Leicester waliotawazwa mabingwa wa EPL mwishoni mwa msimu wa 2015-16, watashuka dimbani wakijivunia rekodi ya kusajili ushindi katika mechi nne kati ya saba zilizopita. Ni matokeo ambayo kwa sasa yanawaweka masogora hao wa Rodgers katika nafasi ya tatu kwa alama 14 jedwalini.

Kwa upande wao, Liverpool wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 21 chini ya kocha Jurgen Klopp. Ni pengo la pointi tano ndilo linalodumu kati yao na mabingwa watetezi Manchester City watakaokuwa kesho wenyeji wa Wolves ya mkufunzi Nuno Espirito ugani Etihad.

Man-City watazikosa huduma za kiungo wao matata Kevin De Bruyne katika mchuano huo dhidi ya Wolves ambao wamekuwa wakisuasua pakubwa katika kampeni za msimu huu. Kikosi hicho cha Espirito kwa sasa kinashikilia nafasi ya 13 jedwalini kwa alama saba sawa na Southampton na Everton.

Kwingineko, Tottenham Hotspur watapania kujinyanyua na kuyaweka kando maruerue ya kichapo cha 7-2 walichopokezwa na Bayern Munich ya Ujerumani katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwanzoni mwa wiki hii.

Chini ya kocha Mauricio Pochettino ambaye tayari anahusishwa na uwezekano wa kuwa mrithi wa Ole Gunnar Solskjaer kambini mwa Manchester United, Tottenham wakiwa wageni wa Brighton uwanjani American Express Community.

Tottenham kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama 11 sawa na Chelsea, Bournemouth na Crystal Palace. Ushindi kwa Tottenham utawapaisha hadi ndani ya mduara wan ne-bora iwapo West Ham watajikwaa dhidi ya Palace, Chelsea wateleze dhidi ya Southampton na Arsenal wazidiwe nguvu na Bournemouth hapo kesho uwanjani Emirates.

Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea wanatazamiwa kuendeleza ubabe wao watakapotua uwanjani St Mary’s kuchuana na Southampton ambao wamepoteza mechi mbili zilizopita mfululizo.

Kwa upande wao, Arsenal nao watapania kuendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani watakapovaana na Bournemouth wanaojivunia msimu wa kuridhisha hadi kufikia sasa msimu huu.

Man-United watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Newcastle United ambao wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya kocha mpya Steve Bruce uwanjani St James’ Park.

West Ham watakuwa wenyeji wa Palace uwanjani London wakilenga kuimarisha zaidi nafasi yao ndani ya mduara wa nane-bora. Kufikia sasa, West Ham ya kocha Manuel Pellegrini wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama sawa na Arsenal.

Norwich na Aston Villa waliopandishwa daraja kwa pamoja kushiriki kivumbi cha EPL mwishoni mwa msimu jana, watakuwa

Watford watakuwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ugani Vicarage Road wakiwinda ushindi wao wa kwanza katika EPL msimu huu watakapochuana na limbukeni Sheffield United ambao wamejizolea jumla ya alama nane kutokana na mechi saba zilizopita.

Everton watakuwa na ulazima wa kusajili ushindi dhidi ya Burnley ili kumwepushia presha kocha Marco Silva ambaye ananing’inia pembamba ugani Goodison Park baada ya kupoteza mechi nne kati ya saba zilizopita.

RATIBA

LEO JUMAMOSI

EPL – Brighton na Tottenham (2.30pm), Norwich na Aston Villa (5.00pm), Watford na Sheffield United (5.00pm), Burnley na Everton (5.00pm), Liverpool na Leicester (5.00pm), West Ham na Crystal Palace (7.30pm);

LaLiga – Leganes na Levante (2.00pm), Real Madrid na Granada (5.00pm), Valencia na Alaves (7.30pm), Osasuna na Villarreal (10.00pm);

Serie A – SPAL na Parma (4.00pm), Verona na Sampdoria (7.00pm), Genoa na Milan (9.45pm);

Bundesliga – Paderborn na Mainz (4.30pm), Leverkusen na Leipzig (4.30pm), Freiburg na Dortmund (4.30pm), Bayern na Hoffenheim (4.30pm), Schalke na Cologne (7.30pm)

Ligue 1 – PSG na Angers (6.30pm), Brest na Metz (9.00pm), Nantes na Nice (9.00pm), Montpellier na Monaco (9.00pm), Toulouse na Bordeaux (9.00pm), Dijon na Strasbourg (9.00pm).

 

JUMAPILI

EPL – Southampton na Chelsea (4.00pm), Manchester City na Wolves (4.00pm), Arsenal na Bournemouth (4.00pm), Newcastle na Manchester United (6.30pm);

LaLiga – Mallorca na Espanyol (1.00pm), Celta Vigo na Athletic Bilbao (3.00pm), Valladolid na Atletico Madrid (5.00pm), Real Sociedad na Getafe (7.30pm), Barcelona na Sevilla (10.00pm);

Serie A– Fiorentina na Udinese (1.30pm), Atalanta na Lecce (4.00pm), Roma na Cagliari (4.00pm), Bologna na Lazio (4.00pm), Torino na Napoli (7.00pm), Inter na Juventus (9.45pm);

Bundesliga– Monchengladbach na Augsburg (2.30pm), Wolfsburg na Union Berlin (4.30pm), Eintracht na Werder (7.00pm);

Ligue 1– Lille na Nimes (4.00pm), Rennes na Reims (6.00pm), Saint-Etienne (Lyon (10.00pm).