Michezo

Reds wazuru St Marys jicho likiwa kileleni

April 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

SOUTHAMPTON, uingereza

HUKU Liverpool ikijiandaa kupepetana na Southampton leo, kocha Jurgen Klopp hana wasiwasi kuhusu ukame wa magoli kwa staa Mohamed Salah akisema mshambuliaji huyo raia wa Misri bado ni kati ya silaha muhimu za klabu yake inayofukuzia taji.

Salah, ambaye alitikisa nyavu mara 44 katika msimu wake wa kwanza uwanjani Anfield, amekamilisha mechi nane bila kuona lango, ingawa bado ana mabao 20 katika msimu wa 2018-2019. Alichangia pakubwa katika bao lililozamisha Tottenham Hotspur katika dakika ya mwisho mnamo Jumapili iliopita.

“Kila mtu anazungumzia kuhusu kutofunga kwake kwa mabao katika sijui mechi ngapi, haoneshi kukerwa na matamshi yao. Mimi pia sina wasiwasi,” alisema Klopp mnamo Jumatano.

Ufanisi wa Salah msimu uliopita unamaanisha anamulikwa zaidi na wapinzani katika kipindi hiki, mara nyingi akikabwa na wachezaji wawili.

Hii imekuwa na athari, ingawa, ya kunufaisha wachezaji wenzake, huku Sadio Mane (mabao 20) na Roberto Firmino (14) wakibeba mzigo mkubwa wa kutafutia ‘The Reds’ mabao.

“Wakati mwingine, unahitaji kukabiliana na hali mpya na sidhani kama alihitaji kufanya hivyo,” alisema Klopp kuhusu umuhimu wa Salah kwa ujumla kwa timu yake na jinsi ambavyo amekuwa akikabiliana na kutoachiwa nafasi ya kuonyesha ukatili wake.

“Yeye ni tishio. Anatusaidia sana. Anakabiliana na hali zote mpya vyema.

“Ukiwa na mfungaji mmoja wa magoli, unafikiria pengine unamtegemea sana. Mwaka huu hatutegemei sana mabao ya Salah, lakini bado yuko katika nafasi nzuri ukilinganisha na wachezaji wengine wote.

“Mabao 17 (ligini) ni idadi nzuri, na bado mechi nyingi hazijachezwa. Haijawahi kuwa tatizo. Tuna alama 79, huwezi kufikisha idadi hii kama una matatizo mengi kwenye msimu.”

Liverpool itamenyana na Southampton leo Ijumaa usiku, huku Klopp akiripoti kwamba hakuna hofu kuhusu jeraha dogo alilopata beki Virgil van Dijk katika ushindi dhidi ya Tottenham.

Katika mechi ya leo Ijumaa, Liverpool italenga kuzidisha presha dhidi ya wapinzani wake wakuu Manchester City itakaposhuka uwanjani St Marys kwa mechi yake ya 33.

Vijana wa Klopp hawajafungwa bao na Southampton katika mechi nne zilizopita. Watakuwa wakifukuzia ushindi wao wa nne mfululizo baada ya kunyuka ‘Saints’ 3-0 katika mechi mbili zilizopita uwanjani Anfield na kuwalemea 2-0 walipozuru uwanjani St Marys mara ya mwisho mnamo Februari 11, 2018.

Mara ya mwisho Southampton ilipozoa alama zote dhidi ya Liverpool uwanjani St Mary’s ligini ilikuwa Machi 20 mwaka 2016 ilipowika 3-2.

Mchezaji mkali

Van Dijk, ambaye wakati huo alikuwa mchezaji wa Southampton, sasa ni mmoja wa wachezaji wakali wa Liverpool.

Amekuwa akitegemewa na Klopp kuweka ulinzi mkali katika ngome ya mabingwa hawa mara 18 wa Uingereza wanaotafuta kumaliza ukame wa miaka 29 wa mataji ya ligi.

Nambari 16 Southampton chini ya kocha Ralph Hasenhuttl wanatarajiwa kujituma vilivyo kwa sababu wako alama tano nje ya mduara hatari wa kutemwa.