Michezo

Refa mzoefu kusimamia fainali ya Kabras na KCB

May 16th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

REFA mwenye tajriba pevu na uzoefu mpana katika ulingo wa raga, Moses Ndung’u ameteuliwa na Shirikisho la Raga Nchini (KRU) kusimamia fainali ya Kenya Cup itakayowakutanisha Kabras Sugar na KCB wikendi hii mjini Kakamega.

Ndung’u aliyemiminiwa sifa kuwa mwamuzi wa fainali ya kipute cha Impala Floodlit mwaka 2018, atasaidiwa na Constant Cap na Godwin Karuga.

Wanabenki wa KCB watachuana na Kabras Sugar kwenye fainali inayotarajiwa kuwa ya kusisimua zaidi na funga-kazi ya msimu huu wa 2018-19 ambao umeshuhudia kampeni za haiba kwa kipindi cha majuma 18 jijini Nairobi na katika miji ya Nakuru na Kakamega.

Katika safari yao ya kufuzu kwa fainali, KCB waliwabamiza Kenya Harlequins 46-13 katika uwanja wa Lion’s Den, Nairobi huku wanasukari wa Kabras wakiyazima makali ya Mwamba RFC kwa alama 23-11 katika nusu-fainali ya pili iliyonogeshwa katika uwanja wa Kakamega ambao pia utakuwa mwenyeji wa fainali muhula huu.

Kabras Sugar na KCB watakuwa wakivaana katika fainali ya Kenya Cup kwa mara ya tatu mfululizo.

KCB na Kabras Sugar wamewahi kukutana katika fainali mbili za Kenya Cup huku wanabenki wakiibuka washindi mara mbili kwa kuwapepeta wapinzani wao kwa alama 36-8 mnamo 2017 kisha 29-24 mnamo 2018. KCB walikuwa wenyeji wa michuano yote miwili.

Mwenyeji

Kwa mujibu wa kanuni, timu inayotamalaki kilele cha jedwali mwishoni mwa msimu huwa mwenyeji wa fainali.

KCB ambao walitawala kilele cha jedwali msimu jana, waliandaa fainali katika uwanja wa KCB Sports Club, Ruaraka.

Msimu huu, Kabras walijipa tiketi ya kuwa wenyeji wa fainali baada ya kuwatamalaki wapinzani wao na kuishikilia kilele cha jedwali.

Kabras walitawazwa mabingwa wa Kenya Cup mnamo 2015-16 baada ya kuwatandika Impala 22-5 uwanjani Impala Sports Club na kuwa kikosi cha pili cha raga kutoka nje ya Nairobi kunyanyua ufalme wa Kenya Cup.

Nakuru ambayo ilikuwa klabu ya kwanza, ilitawazwa mabingwa mnamo 2013 na 2014 mtawalia.

KCB waliwatandika Kabras Sugar 27-3 katika fainali ya Kenya Cup mnamo 2014-15 na kuwakomoa wanasukari hao kwa alama 36-8 katika ushindi uliowashuhudia wakihifadhi ubingwa mnamo 2016-17.