Michezo

Refa wa raga kutoka Afrika Kusini kusimamia KCB ikikabiliana na Kabras

March 21st, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

RAIA wa Afrika Kusini, Archie Sehlako ameteuliwa kupuliza kipenga katika fainali ya Ligi Kuu ya Raga ya Kenya kati ya mabingwa watetezi KCB na mabingwa wa mwaka 2016 Kabras Sugar hapo Machi 24, 2018.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) limetangaza kwamba Sehlako, ambaye amefanya kazi ya kusimamia mechi za raga tangu mwaka 2004, atasaidiwa na Wakenya Victor Oduor na Beryl Akinyi.

Sehlako ni mmoja wa marefa waliosimamia mechi wakati Afrika iliandaa mashindano ya dunia ya chipukizi (JWRT) kwa mara ya kwanza kabisa jijini Nairobi mwaka 2009. Oduor pia ana ujuzi katika ulingo wa dunia. Alisimamia mashindano ya JWRT mwaka 2016.

Charles Mbogo atakuwa kamishna kwenye fainali kati ya KCB na Kabras nao George Mbaye na Dan Ndaba watakuwa majaji.

Mechi hii itapigiwa katika uwanja wa nyumbani wa KCB mtaani Ruaraka, Nairobi.

KCB, ambayo ilimaliza msimu wa kawaida katika nafasi ya kwanza, iliingia fainali kwa kuaibisha Impala Saracens 15-0 katika nusu-fainali Machi 17. Kabras Sugar ilikamilisha msimu wa kawaida katika nafasi ya tatu na kulazimika kusakata mechi mbili kabla ya kufika fainali. Ililemea Strathmore Leos 43-13 Machi 10 na kuingia nusu-fainali. Ilikunyuka Homeboyz 29-13 katika nusu-fainali Machi 17.